Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CHAUKIDU: Ujio wa Tuzo ya Kiswahili ya Mwalimu Nyerere watangazwa

CHAUKIDU: Ujio wa Tuzo ya Kiswahili ya Mwalimu Nyerere watangazwa

Pakua

Baada ya Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuitambua lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kimataifa, sasa Tanzania imetangaza kwamba kwa kushirikiana na nchi nyingine wataanza kutoa Tuzo za Kimataifa za Kiswahili. Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo wa Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro amemweleza hayo mwandishi wa Idhaa hii Leah Mushi aliyehudhuria ufunguzi wa Kongamano la nane la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), uliofanyika leo jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania.

“Mwakani 2024 katika kusherehekea siku ya Kiswahili duniani ambayo inatambulika na UNESCO, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine tutazindua rasmi ‘Tuzo ya kimataifa ya Kiswahili ya Mwalimu Nyerere’ ili kuenzi Kiswahili pamoja na mchango wa mwalimu Nyerere katika kuikuza lugha ya Kiswahili Tanzania, Afrika na duniani kote.”

Waziri Ndumbaro amesema katika tuzo hiyo watu mbalimbali ambao wametoa mchango katika kukuza na kueneza Kiswahili duniani watatambulika nawatapewa tuzo hiyo kwa heshima ya Mwalimu Nyerere. 

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni Rais wa kwanza wa taifa la Tanzania ambaye mara baada ya nchi hiyo kupata uhuru alihakikisha Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya taifa lake na pia kuendelea kukitangaza katika nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki. 

Akiulizwa kwanini tuzo hizo hazitolewi Afrika Mashariki na badala yake zinaenda kutolewa nchini Ufaransa, Waziri huyo wa Utamaduni Sanaa na michezo wa Tanzania amesema “Tuzo hizo zinatolewa Paris kwenye ofisi za UNESCO kwa heshima ya UNESCO kutambua Kiswahili duniani lakini pia kuchagua tarehe 7 ya mwezi wa Saba kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.” 

Kongamano hilo lililozinduliwa leo tarehe 15 Desemba jijini Arusha, litaendelea mpaka tarehe 17 na linahudhuriwa na washiriki kutoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Comorrow, India, Nigeria, Italia, Marekani na Uingereza.

Wahudhuriaji wa kongamano hilo ni pamoja na wawakilishi wa vyama na taasisi zinazokuza lugha za Kiswahili, wakalimani pamoja na walimu wa Kiswahili. 

Rais wa CHAUKIDU Dkt. Fillipo Lubua akizungumza katika uzinduzi huo amewasihi washiriki wa kongamano hilo kuzingatia maendeleo ya kidigitali katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili. 

Dkt. Lubua ambaye pia ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Pittsburg cha nchini Marekani ametoa mafunzo kwa washiriki wa kongamano hili juu ya kutumia Akili unde (AI) ambapo aliwafundisha matumizi bora na yenye maadili ya ChatGPT pamoja na Adobe Express ambao ni mfumo wa kutengeneza picha.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
1'35"
Photo Credit
UN News/Leah Mushi