Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manufaa ya ujumuishaji wa kidijitali na kifedha unapohusishwa na utumaji pesa kutoka nchi moja kwenda nyingine

Manufaa ya ujumuishaji wa kidijitali na kifedha unapohusishwa na utumaji pesa kutoka nchi moja kwenda nyingine

Pakua

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Utumaji fedha kwa familia ambapo maadhimisho ya mwaka huu yanaangazia manufaa ambayo ujumuishaji wa kidijitali na kifedha unapohusishwa na utumaji pesa kutoka nchi moja kwenda nyingine, huzisaidia familia zinazopokea fedha kufikia Malengo yao ya Maendeleo Endelevu, SDGs. 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD, asilimia 14 ya idadi ya watu duniani, au watu bilioni 1, hutuma au kupokea fedha. Hiyo ni sawa na wafanyakazi wahamiaji milioni 200 wanaotuma fedha kwa wanafamilia milioni 800 kote duniani. 

David Casian ni mwanadiaspora wa Tanzania anayeishi kwa miaka mingi nchini Marekani anaeleza namna matumizi ya dijitali yamesaidia sana katika utumaji fedha nyumbani,  “Teknolojia ya kidijitali kitu cha kwanza walichofanya ni kuondoa mambo ya katikati mengi ambayo yalikuwa yanatuzuia na imeleta ufanisi. Katika muda mdogo tu unaweza ukatuma pes ana mpokeaji akapokea kule nyumbani na kama kuna tatizo la haraka likatatuliwa. Kwa hiyo hivi ni vitu vya muhimu sana tunapenda dijitali kwa sababu kweli imeleta mapinduzi makubwa na tumeweza kufanya mambo mengi kwa wakati mchache.” 

Aidha Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa mwaka jana 2022, utumaji fedha kimataifa kwa mataifa ya kipato cha chini na cha kati ulifikia dola bilioni 626.  

Wastani wa kila mwezi wa dola za Marekani 200 hadi 300 zinazotumwa na wafanyakazi wahamiaji husaidia familia nyingi duniani kote na mwanadiaspora huyu David Casian ni shuhuda wa hilo, “Pesa tunazotuma nyumbani zinasaidia wanafamili kwa upande wa mmoja mmoja lakini pia zinasaidia jamii nzima ya watu wetu. Mtu anaweza akawa anaumwa ukatuma pesa akaweza kutibiwa. Ukatuma pesa mtoto amerudishwa kwa ada shuleni unatuma. Unatuma pesa kwa ajili ya mambo ya uchumi labda mtu anahitaji hela kwa ajili ya kufungua kabiashara kidogo ili aweze kujikimu na hii inasaidia kuchangia uchumi wa mtu mmoja mmoja na vile vile kwa taifa kuijumla. Kwa hiyo ni kitu kizuri na ni kitu cha kukiendeleza na kushukuru kwamba dijitali kwakweli imeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya utumaji pesa.” 

Audio Duration
2'23"
Photo Credit
Picha-IFAD