Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO imetoa onyo kwamba matumizi ya vikoleza utamu visivyo sukari hayapunguzi uzito

WHO imetoa onyo kwamba matumizi ya vikoleza utamu visivyo sukari hayapunguzi uzito

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, hii leo limetoa mwongozo unaoshauri watu wasitumie vikoleza utamu visivyo sukari halisia (NSS) kwa lengo la kupunguza uzito na kuepusha magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inasema mwongozo huo unafuatia mapitio ya ushahidi unaodokeza kwamba kutumia sukari isiyo halisia kwa ajili ya kupunguza uzito hauna manufaa ya muda mrefu katika kupunguza mafuta mwilini miongoni mwa watoto na watu wazima. 

Sukari hizo zisizo halisia na ambazo zinatumika ni pamoja na aspartame, advantame, cyclamates, neotame, saccharin, sucralose na stevia. 

Kitu kibaya zaidi ambacho mapitio hayo yamebaini ni kwamba sukari hizo zisizo halisia zinaongeza hatari ya kupata uognjwa wa kisukari aina ya 2, magonjwa ya moyo na vifo miongoni mwa watu wazima. 

Mkurugenzi wa WHO Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula Dkt. Francesco Branca amesema kuacha kutumia sukari ya kawaida na badala yake kutumia sukari zisizo halisia kwa muda mrefu hakusaidii kupunguza uzito. 

Amesema “watu wanapaswa kufikiria njia mbadala za kupunguza matumizi ya sukari kwa kula vyakula vyenye sukari ya asili kama vile matunda au vinywaji na vyakula visivyo na sukari.” 

Amesema “vikoleza utamu visivyo na sukari havina lishe yoyote. Watu wapunguze vyakula vitamu kwenye mlo wao tangu utotoni ili kuimarisha afya zao.” 

WHO inasema pendekezo hilo linahusu watu wote isipokuwa wale wanaougua kisukari. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Photo Credit
WHO/Christopher Black