Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa Monkyepox au Ndui ya Nyani wabadilishwa jina na kuwa MPOX

Ugonjwa wa Monkyepox au Ndui ya Nyani wabadilishwa jina na kuwa MPOX

Pakua

Baada ya mfululizo wa mashauriano na wataalamu wa kimataifa, hatimaye shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO litaanza kutumia jina MPOX badala ya Monkeypox au homa ya Ndui ya Nyani kufuatia mapendekezo ya kubadilishwa kwa jina hilo kwa maelezo ya kwamba lilikuwa linasababisha mambo kadhaa ikiwemo unyanyapaa. Flora Nducha na maelezo zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi, mabadiliko hayo yanaanza rasmi leo lakini majina  hayo mawili MPOX na Monkeypox au Ndui ya Nyani, yatatumika kwa pamoja kwa kipindi cha mwaka mmoja na kisha Monkeypox au Ndui ya Nyani litaondolewa.

WHO inasema ndui ya nyani ilipoibuka mapema mwaka huu na kusambaa katika maeneo ambayo awali ugonjwa huo haukuweko, lugha yenye misingi ya ubaguzi wa rangi nay a unyanyapaa ilienea mtandaoni na kwenye maeneo mengine na katika jamii, na kisha ripoti hizo kuwasilishwa WHO.

Katika mikutano kadhaa, iwe ya uso kwa uso au mtandaoni, watu kadhaa binafsi na nchi waliwasilisha hofu yao na kuomba WHO ipendekeze njia ya kubadilisha jina.

Kubadili au kupatia jina ugonjwa hufanyika kwa nadra sana kwa ugonjwa ambao tayari uko na ni wajibu wa WHO kwa mujibu wa Mfumo wa Kimataifa wa kupangia majina magonjwa, ICD na jukwaa la kimataifa la kupangia majina kupitia mchakato wa mashauriano unaojumuisha nchi wanachama wa WHO.

Baada ya mchakaot huo uliomshirikisha pia Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus, WHO ndio imepitisha mabadiliko hayo na ili kuondoa mkanganyiko wa jina katikati ya mlipuko, ndio  maana yatatumika pamoja kwa mwaka mmoja na kisha Monkeypox kuondolewa.

Kwa mujibu wa WHO, mchakato wa kubadiliha jina ugonjwa huchukua miaka kadhaa, lakini kwa Monkeypox mchakato umeharakishwa kwa kuzingatia kanuni zinazotakiwa,

WHO inasema hoja ya matumizi ya jina lina MPOX katika lugha nyingine lilijadiliwa na iwapo kutatokea mkanganyiko wowote, hoja itajadiliwa kupitia mchakato ulioko kwa uratibu na mamlaka za serikali na vyama vya kitabibu.

Shirika hilo limesema litatumia MPOX katika mawasiliano yake na limesihi watu wengine nao kufanya hivyo ili kupunguza athari hasi za matumizi ya Monkeypox na kupitishwa kwa jina jipya.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration
2'24"
Photo Credit
© Harun Tulunay