Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watafiti msifungie tafiti zenu, chapisheni na sambazeni- Dkt. Chang'a

Watafiti msifungie tafiti zenu, chapisheni na sambazeni- Dkt. Chang'a

Pakua

Mkurugenzi wa masuala ya utafiti na matumizi ya hali ya hewa kutoka Mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania TMA Dr. Ladislaus Chang'a amesema ni vyema wataalamu wa Afrika wakaongeza kasi katika kufanya tafiti na kuzichapisha katika majarida ya kimataifa ili tafiti zao ziweze kutumika katika utungaji wa será za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Chang’a ameyasema hayo akiwa Sharm el-Sheikh nchini Misri kunakofanyika mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27

Mkurugenzi huyo ambaye katika Mkutano huo wa COP27 ni mwenyekiti wa kusimamia majadiliano ya kuhusiana na masuala ya sayansi pamoja na uangazi wa hali ya hewa amehojiwa na Joyce Shebe mwandishi wa Clouds FM ambayo ni redio washirika wetu na kusema kwa sasa matukio yanaongezeka kwa ukubwa na wingi.

“Maamuzi yoyote yanayofanyika katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanakuwa yanatokana na matokeo ya kisayansi na vile vile yanatokana na uangazi ambapo ni muhimu kwa ajili ya kutambua na kukabiliana na changamoto za hali ya hewa hususan matukio ya hali mbaya ya hewa ambayo yanaendelea kuongezeka kwa idadi na ukubwa.”

Je, Afrika inafanya tafiti za kutosha?

“Tafiti zinafanyika lakini hazitoshi, na ndio maana tunaendelea kusisitiza watafiti wetu na wataalamu wetu waendelee kuongeza kasi na tija katika kufanya tafiti na hususan katika kuhakikisha kwamba tunachapisha tafiti hizo katika majarida ya kimataifa ambapo ndipo yanapoweza kuzingatiwa katika kutengeneza será za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kidunia na katika ukanda wa Afrika.”

Je kuna umuhimu wa kuzingatia utafiti?

“ Umuhimu ni mkubwa kwasababu maamuzi yoyote lazima yatokane na matokeo ya kisayansi ili yaweze kuwa na tija na ufanisi, mathalani kumekuwa na ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa ambayo yanajumuisha mvua kubwa za muda mfupi ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa. Kwahivyo ni vyema jamii na dunia ikajua haya matukio yapo namna gani katika sehemu mbalimbali za dunia, na wakati gani ambapo yanaongezeka zaidi na hicho kiwango kikoje, hii itasaidia tunapopanga mipango mathalani ya kujenga barabara au madaraja basi tuweze kuzingatia ukubwa na ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo mvua kubwa, upepo mkali na kadhalika.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Joyce Shebe
Audio Duration
2'57"
Photo Credit
Unsplash/Matt Palmer