Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taka za plastiki zageuka lulu Haiti

Taka za plastiki zageuka lulu Haiti

Pakua

Miradi mbalimbali ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira inasaidia kuifanya dunia kuwa sehemu salama. Nchini Haiti Shirika la Benki ya plastiki linaendesha mradi wa kukusanya plastiki ikiwa ni moja ya njia za kuboresha afya ya na pia ni chanzo cha mapato kwa wakusanyaji taka. Leah Mushi na maelezo zaidi.

Plastiki zinaharibu sayari yetu, zinapokusanywa na kutumika tena zinasaidia kukata mnyororo wa uharibifu wa mazingira na hii ni njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ukusanyaji wa taka za plastiki kutoka kwenye mazingira unasaidia kuondoa plastiki ambazo hufanyika kama mazalia ya viumbe vinavyobeba magonjwa kama vile mbu, kusaidia kupunguza kuenea kwa malaria, homa ya dengue na kipindupindu. Ndege warukao pia huathirika pale wanapokula taka za plastiki wakidhani ni mizoga.

Richardson Gustav ni meneja wa kituo cha kukusanya taka wa shirika la benki ya plastiki nchini Haiti na anasema, “tatizo la uchafuzi wa mazingira nchini Haiti ni kwamba watu hawatambui thamani ya plastiki na hawatambui kwamba kwamba wanaposhika plastiki mikononi mwao hizo ni fedha, na hapo ndio shirika letu la Benki ya plastiki linakuja na kuwahamasisha watu kukusanya taka za plastiki na kuzileta katika vituo vya kukusanya taka ili wajipatie fedha papo hapo.”

Jean Michelet ni mkusanyaji taka za plastiki na anafunguka kuwa, ‘nilikuwa na bustani yangu lakini mvua kubwa ilinyesha na kuharibu mazao yangu. Kisha nikagundua hii kazi ya kukusanya plastiki na nikaona inanifaa, ninachotakiwa ni kukusanya plastiki na kuzileta hapa. »

Kauli yake inaungwa mkono na Pierre Sonel naye pia ni mkusanyaji plastiki akisema, “lengo la programu hii ni kuboresha afya zetu, tunakusanya plastiki kila siku asubuhi n anchi yetu inakuwa safi, na kazi hiyo inaniingizia kipato na kuboresha maisha ya watu na hii ndio sababu tunakusanya plastiki.’

Shaun Frankson ni Mkurugenzi mwenza wa Shirika la Benki ya Plastiki anaeleza nini kinafanyika baada ya plastiki kuletwa katika vituo vya ukusanyaji. Anasema, "tunazikusanya plastiki kuzichakata na kisha kuziuza kwenye makampuni makubwa ya plastiki duniani ili waweze kuzitumia katika bidhaa zao badala ya kutengeneza plastiki mpya. Ni plastiki za kijamii, ni plastiki zinazosaidia kuondoa plastiki kwenye bahari wakati huohuo zikiboresha maisha ya wakusanyaji wa plastiki. »

Mradi huu wa benki ya plastiki unalenga kusaidia wananchi wa Haiti na kadri kunapokuwa na uhitaji mkubwa wa plastiki hizi kutoka kwenye makampuni ya kimataifa inamaana wananchi wengi wa Haiti wanajipatia kipato kupitia fedha wanazopata baada ya kukusanya plastiki.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'49"
Photo Credit
UNFCCC