Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi, unyanyasaji pahala pa kazi pamoja na COVID-19 vyatikisa afya ya akili ya wafanyakazi- Ripoti

Ubaguzi, unyanyasaji pahala pa kazi pamoja na COVID-19 vyatikisa afya ya akili ya wafanyakazi- Ripoti

Pakua

Hatua Madhubuti zinahitajika ili kukabiliana na changamoto za afya ya akili miongoni mwa wafanyakazi , kwa mujibu wa wito mpya  wa pamoja uliotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO na lile la kazi duniani ILO. Taarifa ya Anold Kayanda inafafanua zaidi.

Machapisho mawili ambayo yote yanalenga ujumbe mmoja wa kushughulikia changamoto ya afya ya akili kazini  ambayo ni muongozo mpya wa kimataifa wa WHO kuhusu afya ya akili na uwajibikaji kazini na tamko la pamoja la kisera la WHO na ILO, yanakadiria kwamba takriban siku bilioni 12 za kazi hupotea kila mwaka kutokana na matatizo ya msongo wa mawazo na wasiwasi vinaougharimu uchumi wa dunia karibu dola trilioni 1. 

Mwongozo huo mpya wa kimataifa wa WHO unapendekeza hatua za kukabiliana na hatari ya afya ya akili kama vile kudhibiti mzigo mkubwa wa kazi, tabia mbaya na mambo mengine ambayo husababisha adha kazini.  

Kwa mara ya kwanza WHO inapendekeza mafunzo ya mameneja, ili kuwajengea uwezo wa kuzuia mazingira ya kazi yenye kuongeza shinikizo na kushughulikia ipasavyo wafanyakazi walio katika changamoto. 

WHO imesema kazi huongeza changamoto za kijamii ambazo zinaathiri vibaya afya ya akili. Masuala kama ya ubaguzi na ukosefu wa usawa, uonevu na unyanyasaji wa kisaikolojia ni malalamiko makubwa ya unyanyasaji wa mahali pa kazi ambayo yana athari mbaya kwa afya ya akili  lakini kujadili au kuzungumzia masuala ya afya ya akili bado ni mwiko katika mipangilio ya kazi ulimwenguni kote. 

Mwongozo huo pia unapendekeza njia bora zaidi za kushughulikia mahitaji ya wafanyikazi walio na changamoto za afya ya akili, kama kupendekeza hatua zitakazowasaidia kurejea kazini na kwa watu walio na hali mbaya ya afya ya akili pia muhimu zaidi, miongozo inataka uingiliaji kati unaolenga kulinda afya ya akili ya wahudumu wa afya,  wa kibinadamu na wa dharura. 

Kwa mujibu wa Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa WHO "Ni wakati wa kuzingatia athari mbaya ambazo kazi inaweza kuwa nazo kwa afya yetu ya akili. Ustawi wa mtu binafsi ni sababu tosha ya kuchukua hatua, lakini afya mbaya ya akili inaweza pia kuwa na athari ya kudhoofisha utendaji kazi na tija ya mtu. Miongozo hii mipya inaweza kusaidia kuzuia tamaduni na hali mbaya za kazi na kutoa ulinzi unaohitajika sana wa afya ya akili na usaidizi kwa watu wanaofanya kazi.” 

Nalo tamko la pamoja la kisera la WHO na ILO linafafanua miongozo hiyo ya WHO katika suala la mikakati ya kiutendaji kwa serikali, waajiri na wafanyakazi, na mashirika yao, katika sekta za umma na za kibinafsi.  

Lengo ni kusaidia uzuiaji wa hatari za afya ya akili, kulinda na kukuza afya ya akili kazini, na kusaidia wale walio na matatizo ya afya ya akili, ili waweze kushiriki na kustawi katika ulimwengu wa kazi.  

 Akisisitiza kuhusu hilo Guy Ryder, mkurugenzi mkuu wa ILO amesema "Watu wanatumia sehemu kubwa ya maisha yao kazini hivyo mazingira salama na yenye afya ya kufanya kazi ni muhimu. Tunahitaji kuwekeza ili kujenga utamaduni wa kuzuia matatizo ya afya ya akili kazini, kuunda upya mazingira ya kazi ili kukomesha unyanyapaa na kutengwa kwa jamii, na kuhakikisha wafanyakazi walio na matatizo ya afya ya akili wanahisi kulindwa na kuungwa mkono.” 

WHO na ILO wamesema mwaka 2020, serikali ulimwenguni kote zilitumia wastani wa asilimia 2% tu ya bajeti zake za afya kwa ajili ya afya ya akili, huku nchi za kipato cha chini zikitenga chini ya 1% ya bajeti zake kwa ajili ya tatizo hilo. 

Audio Credit
Flora Nducha/Anold Kayanda
Audio Duration
3'26"
Photo Credit
Unsplash/Eric Ward