Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu tunawapatia watoto iwawezesha kukabili changamoto za sasa - Garnier

Elimu tunawapatia watoto iwawezesha kukabili changamoto za sasa - Garnier

Pakua

Ingawa msemo wa haki ya binadamu umezoelekea, hakuna haki ya binadamu yoyote ambayo imetolewa bure bila kupiganiwa, vivyo hivyo inapaswa kuwa kwa elimu, amesema Leonardo Garnier, Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkutano wa Ngazi ya juu wa Umoja wa MAtaifa kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu duniani, mkutano unaoanza Ijumaa hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo wa ngazi ya juu unafanyika kwa siku tatu ambapo Leonardo Garnier akiwa ni mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu mkutano huo anasema ni dhahiri shairi elimu inapitia janga mahsusi na gumu.

Akihojiwa na UN News jijini New York, Marekani kuelekea mkutano huo, amesema, "changamoto ya kuipata. Mamilioni  ya watoto hawako shuleni, lakini pia ni janga kwa minajili ya kujifunza: wengi walio shuleni hawajifunzi hata yale mambo ya msingi. Na vile vile ni janga la kufaa kwa hicho wanachojifunza. Je wanajifunza wanachohitaji kujifunza kwa dunia ya sasa inayobadilika, halikadhalika uchumi tunamoishi.”
 

Amesema maswali hayo ndio msingi wa mkutano huo wa ngazi ya juu, maswali ambayo yasipojibiwa kwa kufanyia marekebisho mfumo wa elimu, Dunia itarudia kilichotokea miaka ya themanini, ikiwemo kupunguza bajeti za elimu na watoto wengi kutokuwa shuleni.

Bwana Garnier amesema, "kwa hivyo watapoteza kwa ajira ambayo wanaweza kufanya, lakini pia aina ya wakazi wa Dunia ambao watakuwa katika dunia ya sasa. Hawatakuwa tayari kuishi pamoja kwenye dunia yenye changamoto nyingi, kukwepa mizozo na kukabili changamoto kama hizi za sasa za tabianchi.Tunataka elimu ya kukabili hayo kwa sababu tunapenda kusema ujumuishaji ni haki ya binadamu lakini tukumbuke hakuna haki ya binadamu imepatikana kwa neema tu.”

Bwana Garnier amesema wale wanaoenguliwa katika elimu watapigania haki yao, kwa hiyo viongozi wa kisiasa lazima wasikilize na wachukue hatua.

Audio Duration
2'
Photo Credit
© UNICEF/Frank Dejongh