Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hisabati inawezekana pia kwa watoto wa kike wakipatiwa fursa kama wavulana- UNICEF

Hisabati inawezekana pia kwa watoto wa kike wakipatiwa fursa kama wavulana- UNICEF

Pakua

Kuelekea mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Marekebisho ya Mfumo wa Elimu, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ulimwenguni UNICEF limetoa ripoti inayoonya kuwa viwango vya chini vya ustadi wa somo la hisabati hususani kwa wasichana, vinadhoofisha uwezo wa watoto hao kujifunza, kujiendeleza na kuwa na maendeleo. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi

“ Ninapenda kemia kwa sababu ikiwa kuna nafasi ya mimi kuendelea na elimu yangu, ningependa kusomea udaktari." Ndivyo anavyosema Chantal Atovura, mwanafunzi huyu mkimbizi kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC akiwa nchini Sudan Kusini.

Lakini ndoto za wasichana kama Chantal zinaweza kutokomea iwapo hatua hazitachukuliwa haraka na kila serikali kukomesha ubaguzi wa kijinsia ambao ripoti mpya iliyotolewa leo na UNICEF inawaweka wasichana duniani nafasi ya nyuma katika somo la hisabati ikilinganishwa na wavulana.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo jijini New York Marekani ikipatiwa jina: Tatua mlinganyo: kuwasaidia wasichana na wavulana kujifunza hisabati inatokana na utafiti kwenye zaidi ya nchi 100 duniani zenye uchumi wa chini na wakati na imegunduliwa kuwa wavulana wana uwezo wa hadi mara 1.3 zaidi ya kupata ujuzi wa hisabati kuliko wasichana na sababu kubwa ni mtazamano hasi wa kijinsia walionao walimu, wazazi na hata marika husika kuwa wasichana wanashindwa kuelewa na hii hushusha morali ya wasichana kujifunza na mwisho kufeli.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell akizindua ripoti hiyo amesema “Wasichana wana uwezo sawa wa kujifunza hisabati kama wavulana,  wanachokosa ni fursa sawa ya kupata ujuzi huo muhimu".

Soma la hisabati ni muhimu kwenye maisha kwa kuwa linasaidia kuimarisha kumbukumbu, ufahamu, na uchanganuzi, na hivyo kuboresha uwezo wa watoto wa kuwa wabunifu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF akishauri nini kifanyike amesema "Tunahitaji kuondoa dhana potofu za kijinsia na kanuni zinazowarudisha nyuma wasichana na kuongeza juhudi kusaidia kila mtoto kujifunza ujuzi wa kimsingi anaohitaji ili kufaulu shuleni na maishani."

UNICEF inatoa wito kwa serikali kuhakikisha inafikisha elimu bora kwa watoto wote na kwamba juhudi na uwekezaji mpya unahitajika ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha upya na kuwabakisha watoto wote shuleni ili wapate masomo ya ziada, kusaidia walimu kwa kuwapa zana wanazohitaji, na kuhakikisha kuwa shule zinaweka mazingira salama na yenye utayari wa kutoa msaada kwa watoto wote  ili wawe tayari kujifunza.

Sababu nyingine zilizo ainishwa katika ripoti hiyo zinazo wafanya wasichana kuwa nyuma ya wavulana kwenye somo la hisabati ni pamoja na uwezo wa kiuchumi wa familia, watoto kupata masomo ya awali,  pamoja na athari za janga la COVID19.

 

 

Audio Credit
Flora Nducha/ Leah Mushi
Audio Duration
2'54"
Photo Credit
UNHCR/Egor Dubrovsky