Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi na utekaji vinachochea watoto wengi kutokuwa shuleni Afrika Magharibi:UNESCO

Mashambulizi na utekaji vinachochea watoto wengi kutokuwa shuleni Afrika Magharibi:UNESCO

Watoto, vijana na vijana balehe milioni hamsini na saba wanakwama kwenda shule katika ukanda wa Afrika ya Kati na Magharibi, ambayo ni asilimia 24.1 ya watu milioni 236 ambao hawaendi shule duniani kote, linaonya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) katika ripoti inayolenga kuonesha hali ilivyo wakati leo ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kulinda Elimu dhidi ya Mashambulizi. Taarifa inayosomwa na Anold Kayanda inaeleza zaidi.  

(Taarifa ya Anold Kayanda) 

Idadi ya shule zilizofungwa imeongezeka katika nchi nane za eneo la Afrika ya Kati na Magharibi, huku zaidi ya shule 12,400 zikifungwa kufikia mwisho wa mwaka wa shule wa 2021-22, inasema ripoti ikiongeza kuwa nchini Burkina Faso, Chad, Mali na Niger zaidi ya nusu ya watoto na vijana wote hawana fursa ya kupata elimu. 

Katika mwaka uliopita wa shule, idadi ya shule zilizofungwa iliongezeka kwa asilimia 66 katika eneo la Sahel ya Kati pekee. Shule ama ndizo zinazolengwa moja kwa moja na makundi yasiyo ya serikali ambayo yamejihami kwa silaha au wanafunzi wanazitelekeza shule kwa hofu ya mashambulizi. Vurugu pia hulazimisha jamii nzima kupoteza rasilimali zao na kukimbia, na hivyo kuzuia watoto na vijana kupata elimu. 

Millicent Mutuli, Mkurugenzi wa Ofisi ya UNHCR Kanda ya Afrika Magharibi na Kati anasema, "cha kusikitisha ni kwamba taasisi za masomo hazijaepushwa na mashambulizi ya makundi yenye silaha. Kudumisha upatikanaji wa elimu salama na bora kwa watoto wote, ikiwa ni pamoja na wakimbizi, ni muhimu."  

Naye Maureen Magee, Mkurugenzi wa Kanda wa Baraza na wakimbizi la Norway, NRC katika eneo la Afrika ya Kati na Magharibi ananukuliwa akisema kuwa, "kila mtoto aliye nje ya shule, kila siku ya kujifunza inayopotea, ni tofali moja pungufu ili kujenga amani na ustawi katika ukanda huu. Katika muktadha huu wa vurugu zisizoisha na familia kuhamishwa mara kwa mara kutoka katika makazi yao, viongozi wa Kanda ya Afrika ya Kati na Magharibi lazima wafanye kila wawezalo ili kuhakikisha utekelezaji kamili wa Azimio la Shule Salama na kulinda haki ya kila mtoto kwenda shule." 

Mashirika yote matatu yanatoa wito kwa serikali, vikosi vya kijeshi, wahusika wengine kwenye mizozo na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za pamoja ili kukomesha mashambulizi na vitisho dhidi ya shule, wanafunzi na walimu, pamoja na kuongeza uungaji mkono endelevu wa elimu bora kwa kila mtoto katika kanda. 

Pakua
Audio Credit
UN News/ Anold Kayanda
Audio Duration
2'30"
Photo Credit
© UNICEF Frank Dejongh