Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria ichukue mkondo wake kuepusha chuki baina ya walinda amani wa UN na raia DRC - Jean-Pierre Lacroix

Sheria ichukue mkondo wake kuepusha chuki baina ya walinda amani wa UN na raia DRC - Jean-Pierre Lacroix

Pakua

Viongozi wa Umoja wa mataifa pamoja na serikali ya Jamhuri ya Kidemoktrais ya Congo, DRC wametoa heshima zao za mwisho kwa walinda amani watano wa kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO waliokufa wakati wa maandamano na uvamizi wa vituo vya ujumbe huo huko Goma na Butembo jimboni Kivu Kaskazini. Walinda amani hao wanatoka Morocco na India ambapo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Bintou Keita amesema MONUSCO iko tayari kwa mazungumzo ya amani ili kuendeleza na kudumisha amani nchini humo. Taarifa iliyoandaliwa na Mwandishi wetu wa DRC, Byobe Malenga inaeleza zaidi.

Tukio la kuaga walinda amani hao wa Umoja wa Mataifa limefanyika mbele ya Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC Bintou Keita.   

Bwana Lacroix amesema walinda amani hao mashujaa waliokufa wakilinda sio tu Umoja wa Mataifa bali pia raia na kwamba sheria ichukue mkondo wake kuepusha chuki baina ya walinda amani wa UN na raia nchini humo.  

“Kwa hivyo, ingawa tunasikitishwa na kuwapoteza mashujaa wetu hawa watano waliofariki dunia katika huduma ya kulinda amani, kumbukumbu inatuwajibisha sote kuwa na shukrani. Walitenda kazi kwa ushujaa kutulinda na kulinda watu licha ya maandamano kupita kiasi na hila zilizosababisha tukio hili baya. Haki lazima itolewe kwa wenzetu wote wa Umoja wa Mataifa ambao wamepoteza maisha, lakini bila shaka haki lazima itolewe kwa ndugu na dada zetu wote wa DRC ambao wanaendelea kuteseka na vitisho vya vita." Amesema Jean-Pierre Lacroix   

Naye Bintou Keita ambaye pia ni Mkuu wa MONUSCO ameelezea mshikamano wake na rambirambi kwa familia zinazoomboleza na kuthibitisha utayari wa ujumbe huo kupokea ukosoaji na uwazi wake wa mazungumzo na pande zote DRC zinazotaka kuwasilisha malalamiko yao kwa amani akisema, “MONUSCO inakabiliwa na wimbi la maandamano na uhasama. Ningependa kuthibitisha uwazi wa Monusco na timu nzima ya Monusco kwa ukosoaji wowote na upatikanaji wake wa kufanya mazungumzo na wale wote wanaotaka kueleza malalamiko yao kwa njia ya amani ili kuchangia MONUSCO kuondoka kwa utaratibu na kuwajibika kwa ujumbe wetu.” 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Byobe Malenga
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
UN/Byobe Malenga