Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa DRC waliokuwa Uganda warejea kwao kwa hiyari

Wakimbizi wa DRC waliokuwa Uganda warejea kwao kwa hiyari

Pakua

Wakimbizi 11,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC waliokimbilia nchi jirani ya Uganda hivi karibuni kufuatia machafuko yanayoendelea Mashariki mwa DRC wameanza kurejea nyumbani kwa hiyari na kilichowasukuma ni usemi wa wahenga kuwa nyumbani ni nyumbani.

John Kibego na taarifa kamili 
Nattss…… 
Katika kituo cha mapokezi ya muda ya wakimbizi cha Nyakabande mpakani mwa Uganda na DRC Enoch Twaza mwenye umri wa miaka 50 akiwa na familia yake wako tayari kurejea nyumbani Bunagana Mashariki kwa DRC. 

Watalazimika kutembea mwendo wa kilometa 20 wakiwa na virago vyao na mifugo yao kurejea Congo. Twaza anakumbuka kilichowalazimisha kufungasha virago ya kuja Uganda kusaka usalama 

“Mimi nilisikia milio ya risasi ndio nikakimbia, halafu nilipokimbia nilikuja kwa miguu hadi Nyakabande na baada ya kukaa hapa kwa siku mbili kisha nikasikia nyumbani kumetulia, sasa nimeamua kurudi "

Twanza ni miongoni mwa wakimbizi 11,000 waliochagua kurejea nyumbani lakini kuna wengine wengi walioamua kubaki kwa sababu ya sintofahamu ya mustakbali wao.  Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wakimbizi wanaorejea nyumbani wananya hivyo baada ya maafisa wa usalama wa Uganda na Congo DRC kuwajulisha kwamba ni salama kurejea nyumbani. 

Mapema mwezi Novemba mwaka huu mapigano mapya yalizuka baina ya makundi yenye silaha na vikosi vya serikali ya DRC na kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani ya Uganda kusaka hifadhi.

Mongera Bahiira ana umri wa miaka 60, yeye mkewe na watoto sita kati ya 13 walionao waliikimbia nyumba yao na kubeba walichoweza hadi Bunagana baada ya kijiji cha cha Masisi wilayani Rutshuru jimbo la Kivu Kaskazini kushambuliwa na wanamgambo wenye silaha mwezi Oktoba  
“Sisi tuliona jinsi Congo kulivyo na vita sana, na tukaona kukimbia kila mara na kurudi hatuwezi, sasa ndio tumekuja hapa mikoni mwenu.” 

Naye mkewe Safari Nekuse anasema “Niliugua kwa kubeba mizigo mizito tukikimbiua, nilihisi kama itaniua, pia ninahofia wanangu wakubwa ambao walibaki kijijini masisi.”  Hadi sasa wakimbizi takribani 10,000 kati ya 11,000 waliokimbia hivi karibuni wamesharejea nyumbani na waliosalia ikiwemo familia ya Mongera wamehamishiwa kituo cha Nyakabande kwa msaada wa UNHCR na serikali ya Uganda.

Audio Credit
Flora Nducha / John Kibego
Audio Duration
2'27"
Photo Credit
VIDEO YA UNHCR