Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Tanzania ashauri Umoja wa Mataifa kuwasaidia wakimbizi waliorejea kwao

Rais wa Tanzania ashauri Umoja wa Mataifa kuwasaidia wakimbizi waliorejea kwao

Pakua

Hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR limesema wakimbizi 343 wa Burundi waliokuwa wanaishi nchini Uganda wamerejea nyumbani jana jumatatu na kufanya idadi ya wakimbizi waliorejea nyumbani kwa hiari kwa mwaka huu pekee kufikia zaidi ya 60,000 ambapo takribani nusu yao wamerejea kutoka Tanzania.
Mapema mwezi Septemba mwaka huu akiwa jijini New  York, Marekani kushiriki vikao vya Umoja wa Mataifa, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipozungumza na Idhaa hii ya Kiswahili alisema waliomba mazungumzo na mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNHCR kusaidia nchi ambako wakimbizi wanatoka ili waweze kurejea akitolea mfano Burundi. Rais Samia anaanza kwa kueleza hali ya wakimbizi ilivyo hivi sasa nchini Tanzania.

(Sauti ya Samia)

"Tuna wakimbizi takribani 347,600 na kitu hivi kutoka Burundi.Lakini tua wakimbizi wengine kama 200,000 na hivi kutoka DRC na wengine kama 368 wa mataifa mbalimbali. Hawa wa mataifa mbalimbali hawatupi shida kwa sababu wapo tunajua wapo. Lakini wale ambao wako kwenye makambi pale Kigoma, tuna makambi matatu ya wakimbizi. mwaka juzi tulifanya mazungumzo na tukakubaliana kuwarudisha, sisi na lile shirika linalohudumia wakimbizi, UNHCR, tukakubaliana kuwarudisha nyumbani na tukaanza kazi ya kuwarudisha nyumbani wale wa Burundi. Wa DRC hatuwezi kuwarudisha kwa sababu bado hakujatengamaa vizuri. Lakini Burundi tunashukuru sana Rais Ndayishimiye (Evariste) ameifanya Burundi imeulia, usalama uko wa kutosha na tukaanza kurudisha wakimbizi. Kinachotokea ni nini; wakifika Burundi hawana ardhi hawana nyumba, hawana pa kufikia. Na mapokezi pia wanaonekana kwamba mlienda wapi kwa nini mmerudi. Kwa hivyo wanajikuta hawako mahali pazuri, hawapokewi wanatafuta njia za kurudi tena nyumbani."

Na kwa msingi huo

(Sauti ya Samia)

"Tumeomba mazungumzo na hili shirika (la Umoja wa Mataifa) linalohudumia wakimbizi, lakini pia mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kwamba waende wasaidie kule Burundi, hali itengamae kule Burundi kuwe na mipango yote ya kupokea wakimbizi na kuwafaya waweze kuishi ndani ya nchi yao. Tukiweza kufanya hivyo, tutaweza kuondosha wakimbizi kwetu kurudi kwao. Lakini bila kufanya hivyo wanarudi. Na wanaporudi hatuwezi kuwafukuza kwa sababu tumesaini mikataba ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa kwamba tutapokea na tutatunza wakimbizi."

Tanzania kwa zaidi ya miaka 50 imekuwa kimbilio la wakimbizi wakiwemo wanaotoka Burundi, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC na Rwanda.

TAGS: UNHCR, Samia Suluhu Hassan, Wakimbizi, Burundi, Tanzania

 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'57"
Photo Credit
© UNICEF/Karel Prinsloo