Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu wanawake, amani na usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu wanawake, amani na usalama

Pakua

Muda wa kurudisha nyuma saa ya haki za wanawake umepita, sasa iende mbele- Guterres alieleza Baraza (OVERNIGHT)
 
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu wanawake, amani na usalama ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakati umefika kwa baraza hilo kuonesha kwa vitendo uungaji wake mkono wa harakati za wanawake katika ujenzi na uendelezaji wa amani badala ya kusalia maneno matupu.  Flora Nducha na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Flora Nducha)
 
Guterres amehutubia kikao hicho katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya kutembelea ushoroba mahsusi uliokuwa umepambwa na picha za wanawake walio mstari wa mbele katika kusongesha amani kwenye nchi zao.
 
Katibu Mkuu amesema ushiriki wa wanawake kama hao unazidi kukumbwa na changamoto kubwa ambako katika baadhi ya nchi kama vile Afghanistan na Mali fursa hiyo imebinywa na kwingineko ushiriki wao hata kule ambako Umoja wa Mataifa unaendeleza shughuli za ulinzi na ujenzi wa amani unakumbwa na changamoto na vitisho.
 
Amesema kuongeza uwakilishi na uongozi wa wanawake katika shughuli zote za masuala ya amani za Umoja wa Mataifa ni muhimu ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya umoja huo kwa jamii ambazo zinahudumiwa.
 
(Sauti ya Antonio Guterres)

“Hata hivyo tunahitaji Baraza hili lituunge mkono katika njia tatu- ubia, ulinzi na ushiriki. Mosi ungeni mkono kazi yetu ya kuimarisha ubia wetu na wanawake viongozi na mitandao yao katika jamii ambako Umoja wa Mataifa unafanya kazi ili kusaidia wanawake waleta mabadiliko ya amani na usalama. Wanahitaji kuwa na uwezo wa kushiriki katika michakato ya kina na dhati ya amani na kisiasa”
 
Katibu Mkuu amesema  kwa ulinzi, “tusaidieni kuwalinda wanawake watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati. Mashujaa ambao wameoneshwa katika onesho la picha pale nchi wanatia maisha yao hatarini ili kujenga amnai katika jamii zao. Wanahitaji ulinzi pindi wanapotekeleza kazi hiyo muhimu.”
 
Akifafanua kuhusu ushiriki wa wanawake katika amani na usalama,  Katibu Mkuu amesema “shirikianeni nasi katika kuendeleza ushiriki wa uwiano sawa na wa dhati wa wanawake katika mazungumzo ya amani, na mifumo ya kisiasa wakati nchi zinakuwa katika kipindi cha mpito cha amani.”  
 
Akimaanisha kuwepo na uwiano sawa wa uwakilishi kati ya wanawake na wanaume kuanzia ngazi ya uchaguzi hadi taasisi za uongozi.
 
Wajumbe wa Baraza wamekumbushwa ahadi yao waliyoitoa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed alipohutubia baraza hilo baada ya kurejea Somalia alikoenda kuunga mkono suala la kuwa na asilimia 30 ya wanawake katika chaguzi zijazo ambapo Baraza lilisema litaunga mkono.
 
“Wakati umefika kubadili maneno yenu ya kuunga mkono kuwa vitendo, na siyo tu kwa Somalia bali pia katika nchi zote ambazo zinajadiliwa kwenye Baraza hili.” Amesema Guterres akitamatisha akisema wanawake katu hawatokubali tena haki zao kurejeshwa nyuma na njia pekee ya kuheshimu wanawake majasiri wajenzi wa amani ni kufungua milango na wao waweze kushiriki kwa dhati.
 
TAGS: Wanawake, Amani na Usalama

 

Audio Credit
Assumpta Massoi / Flora Nducha
Audio Duration
3'18"
Photo Credit
MONUSCO