Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DR Congo, machifu wasema mawasiliano ni muhimu kudhibiti machafuko  

DR Congo, machifu wasema mawasiliano ni muhimu kudhibiti machafuko  

Pakua

Mawasiliano na elimu kwa vijana na viongozi wa vijiji na mitaa ni jambo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ili kusaidia vijana kuachana na mawazo potofu na kujiingiza katika magenge ya uhalifu, amesema kiongozi mkuu wa machifu kwenye mji wa Oicha jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC alipokutana na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB, cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO. Kikosi hicho cha 7 cha Tanzania, TANZBATT kilitembelea eneo hilo ambalo mara kwa mara hukumbwa na machafuko na wamekutana na Kasereka Ngereza, Chifu Mkuu wa eneo la Ochia. Luteni Issa Mwakalambo na maelezo zaidi.

Chifu Ngereza anasema, “tungependelea wale machifu walio huku chini waweze kurahisisha namna ya kuwasiliana na vyombo vya usalama. Hata hivyo tunashukuru kuwa hao machifu na hata raia mmoja mmoja kama kuna neno wanatuita na hii inatuonesha kuwa mawasiliano yapo. Sasa kuongeza ile nguvu tunajiuliza je kila mtu anakuwa na chombo hata cha kuwasiliana. Na je yule mwenye chombo ana uwezo wa kuwa na fedha za kuweka humo ndani?” 

Chifu Ngereza akaenda mbali zaidi kuelezea umuhimu wa barabara akisema “barabara ya kuweza kurahisisha kusafirisha magari na pia kwenda huko kwa wepesi.” 

Walinda amani kutoka Indonesia na Tanzania wakikagua barabara huko Beni kabla ya  kuanza kwa ukarabati.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani kutoka Indonesia na Tanzania wakikagua barabara huko Beni kabla ya kuanza kwa ukarabati.

 

Vijana na amani 

Katika mkutano wao pia wamezungumzia suala la kuepusha vijana kutumbukia kwenye mitego ya mapigano akisema, “lakini hii ya kuhusu vijana tutajitahidi, kwa sababu tuliwahi kuwa na vikao vitatu na vijana kuhusu hatari ya kumiliki silaha bila ruhusa. Tulienda Mabasele na Pakanza na tangu ile semina tumewahi kupata silaha tatu zilizorejeshwa.” 

Meja Elibariki Zablon Mollel ni Kaimu Kamanda wa kikosi na mkuu wa operesheni TANZBATT-7 ameeleza lengo la ziara yao akisema ni kujenga uhusiano kati yao na viongozi wa Oicha. Amesema uhusiano na viongozi wa vijiji ni mazuri. 

Mji wa Oicha ni miongoni mwa maeneo ambayo TANZBATT-7 inahudumu kupitia kiteule chake cha Matombo na Meja  Emmanuel Benedict ni Kaimu Kamanda wa kiteule cha Matombo na anafafanua umuhimu wa mawasiliano  akisema, “sisi lengo letu kubwa ni ulinzi wa amani na tunaposema ulinzi wa amani ni pamoja na kushirikisha na raia. Kwa hiyo leo tumekuja kwa Chifu wa Oicha ili tuweze kufanya nao mahusiano na kuboresha uhusiano na watu hawa tunaowalinda.” 

 

Audio Credit
Flora Nducha/Issa Mwakalambo
Sauti
3'7"
Photo Credit
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua