Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: COVID-19 inakumbusha jukumu la mabunge katika kuimarisha jamii

Guterres: COVID-19 inakumbusha jukumu la mabunge katika kuimarisha jamii

Pakua

Katika ujumbe wake hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  anasema kuwa kuliko wakati wowote ule, hivi sasa katika janga la virusi vya Corona au COVID-19, jamii inakumbushwa majukumu muhimu ya mabunge katika kusongesha maleno ya maendeleo endelevu, au SDGs. Taarifa inasomwa na Hilda Phoya

Amesema COVID-19 imedhihirisha umuhimu wa kuwa na mifumo thabiti ya afya na mitandao bora ya hifadhi ya jamii na hivyo, “nasihi mabunge ya nchi kokote pale kutekeleza kwa kina majukumu yao na kusongesha hatua endelevu na jumuishi. Hili liratibiwe kwa pamoja na mashirika ya kiraia ili kuwa na mipango ya kitaifa bila  ubaguzi.”

Miongoni mwa mabunge yaliyoendelea na vikao katikati ya janga la  COVID-19 ni Bunge la Tanzania ambapo wake, Spika Job Ndugai anasema, "tulipata changamoto nyingi ambazo zilisababisha pawe na mabadiliko makubwa ya utendaji kazi ndani ya ukumbi wa bunge na katika mazingira ya kibunge. Ambapo utaratibu wa bunge mtandao ndio ulisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya karatasi katika uendeshaji wetu wa bunge lakini tulichukua hatua nyingi kuweka maeneo mengi ya kuweza kunawa mikono kwa maji tiririka sabuni, kutumia dawa maalum, barakoa na tukaanza kutumia kumbi kadhaa wala sio ukumbi mmoja, ambazo zikawa zinaunganishwa kwa utaratibu wa mikutano ya video"

Na jambo gani basi walilopambana nalo zaidi? Spika Ndugai anasema, "kikubwa ambacho tulipambana nacho ni hofu ambayo waheshimiwa wabunge pamoja na watumishi wa bunge  na wananchi kwa ujumla walikuwa wamepata taarifa za ugonjwa huu ambazo hazikuwa zinaeleweka vizuri na watu walio wengi. Tunamshukuru Mungu pamoja na  hofu hiyo kubwa tuliweza kufanya kazi mwanzo mwisho ambapo tulimaliza shughuli zetu tarehe 16  mwezi wa Juni mwaka 2020. Hakika ugonjwa huu umetingisha sana bunge letu na  umesababisha mabadiliko ambayo yatakaa kwa muda mrefu sana miongoni mwetu na huenda yakawa ni mabadiliko ya moja kwa moja katika namna ya utendaji kazi wetu.Mabadiliko ambayo yaliyo mengi yametupeleka kufanya kazi katika njia za mtandao zaidi kuliko njia ambazo tumekuwa tukizitumia hapo mwanzo."

Audio Credit
Flora Nducha/Hilda Phoya
Audio Duration
2'44"
Photo Credit
UN Photo/Eric Kanalstein