Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndoto ya mkimbizi wa Syria kuwa fundi umeme yatimia huko Ujerumani

Ndoto ya mkimbizi wa Syria kuwa fundi umeme yatimia huko Ujerumani

Pakua

Hatimaye ndoto za mkimbizi kutoka Syria za kutaka kutumia ujuzi wake katika hisabati na fizikia zimetimia huko Ujerumani baada ya kupata kazi katika kampuni ambamo kwayo anatumia stadi zake. Loise Wairimu na ripoti kamili.

Mjini Hamburg,nchini Ujerumani, katika karakana ya treni ya kampuni ya Deutche Bahn.Tunakutana na Mohammad Alkalaf, mkimbizi kutoka Syira mwenye umri wa miaka 28 ambaye hatimaye ametimiza ndoto yake baada ya kuajiriwa kwa nafasi ya uanagezi kwenye kampuni hii ya treni ya kijerumani.

Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Mohammad anasema kuwa

“Nilikuwa nikisaidia kilimo cha mizeituni katika shamba la familia huko Idblib, kaskazini-magharibi mwa Syria. Lakini nilikuwa na ujuzi mkubwa katika hisabati na fizikia na nilitambua kuwa nitaweza kufanya kazi katika kampuni za teknolojia kwa hiyo baada ya kuhitimu sekondari ya juu nilitumai kuwa nitasonga mbele zaidi.”

Hata hivyo vita vilipoibuka Syria ndoto ilianza kuyoyoma na alikimbia nchi hiyo mwaka 2014 akitumai kuungana na kaka yake nchini Sweden, jambo ambalo halikuwezekana lakini mwaka 2017 alipata hifadhi nchini Ujerumani.

Akiwa Ujerumani, Mohammad amejifunza kijerumani na alitamani sana kuwa fundi umeme na alituma maombi 200 ya kazi ,na kwa bahati aliona tangazo la uanagenzi katika  kampuni ya reli ya Deutsche Ban ambapo aliwasilisha ombi na kukubaliwa.

Ulrike Stodt ni mkuu wa mradi wa Chance kwenye kampuni ya Deutsche Bahn.

“Tungependa kuhamasisha kampuni nyingine ziangalie wakimbizi na ziwapatie mafunzo na kuwajumuisha kwenye ajira. Tumekuwa na uzoefu mzuri sana na tumechukua wafanyakazi wapya na hii inalipa,”

Na kwa Mohammad akifaulu mtihani Deutsche Bahn baada ya miaka miwili ya stadi za mafunzo, atakuwa na uwezo wa kuendeleza ndoto yake ya ufundi umeme.

 “Mwanzoni nilipoteza matumaini. Sikuweza kufikiria chochote kuhusu maisha yangu ya baadaye kwa sababu ya vita nchini Syria. Sasa niko kwenye uanagenzi na nina uhakika wa ajira. Sasa ninaweza tena kufikiria mustakhbali wangu na nina matumaini zaidi.”

Audio Duration
2'8"
Photo Credit
UN News