Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 ni madhila juu ya madhili kwa watoto DRC

COVID-19 ni madhila juu ya madhili kwa watoto DRC

Pakua

Mfumo wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, unahitaji msaada wa haraka wakati huu ukilemewa na magonjwa ya surua na kipindupindu yanayokatili maisha ya maelfu ya watoto pamoja na tishio la janga jipya la virusi vya Corona COVID-19. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.
 (TAARIFA YA JASON NYAKUNDI)
 Janga hilo ni dhahiri na miongoni mwa waliokumbwa nalo ni Mama Bwanga mkazi wa eneo la Mikonga kwenye viunga vya Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Alikuwa na watoto watano lakini wawili wao walifariki dunia kutokana na surua, mmoja alifariki na umri wa miaka minne na mwingine mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu alifariki dunia wiki moja baadaye, na anasema,
(Sauti ya Mama Bwanga)
“Kwanza alikuwa na vipele mwili mzima, kisha macho yake yalikuwa mekundu, alikuwa hawezi kula. Walimpatia dawa lakini hakupata nafuu, alifariki dunia na umri wa miaka minne. Mtoto wa pili alikufa wiki moja baadaye, naye pia Jumanne. Ili kusahau machungu, nazungumza na watu lakini majonzi yanarejea, nalia. Tulikosa fedha na taarifa kuhusu chanjo ya surua.”
Sasa kumbukizi yake ni picha tu ambapo UNICEF katika ripoti yake ya leo kuhusu surua na kipindupindu DRC inasema kwamba, juhudi za kukabiliana na Ebola Mashariki mwa nchi hiyo zimebadili mtazamo na kupeleka rasilimali katika janga hilo kutoka kwenye vituo vingine vya afya ambavyo tayari vimezidiwa kwa kukabiliana na magonjwa mengi ya mlipuko.
 
Tangu mwanzo wa mwaka 2019 mlipuko wa surua ambao ni mbaya zaidi kushuhudiwa duniani umekatili maisha ya watoto zaidi ya 5,300 wenye umri wa chini ya miaka mitano huku pia kukiwa na wagonjwa 31,000 wa kipindupindu.
 
Kana kwamba maradhi hayo hayatoshi ripoti inasema "sasa mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 unasambaa kwa kasi na kutoa mtihani mkubwa kwa nchi hiyo ambayo imeelezwa kuwa katika hatari zaidi barani Afrika.”
UNICEF imeongeza kuwa hali hii ni sawa na kuweka msumari wa moto juu ya kidonda kwani katika vituo vya afya vya umma, vifaa, wahudumu wenye ujuzi na fedha ni haba. Vituo vingi vinakosa hata huduma za msingi za maji na usafi na kiwango cha chanjo ambacho kilikuwa chini sasa kimeshuka zaidi kwa mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNICEF takriban watoto milioni 3.3 nchini DRC wanakosa huduma za msingi za afya, huku katika nchi nzima watoto milioni 9.1 karibu mtoto 1 kati ya 5 waliochini ya miaka 18 anahitaji msaada wa kibinadamu.
UNICEF imeonya kwamba "endapo vituo vya afya havitapata njia ya kufikisha chanjo, lishe na huduma zingine za msingi ikiwemo kwenye maeneo ya vijijini nchini humo basi tuna hatari ya kushuhudia maisha na mustakabali wa watoto wengi wa Congo ukisambaratishwa na magonjwa yanayoweza kuzuilika."

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Jason Nyakundi
Sauti
2'54"
Photo Credit
WHO