Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ibara ya 6 ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi bado kizungumkuti- Andersen

Ibara ya 6 ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi bado kizungumkuti- Andersen

Pakua

Mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP25 umeanza leo mjini Madrid, Hispania, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa ziara zake katika mataifa yaliyokumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi yameimarisha harakati zake za kusaka suluhu ya janga hilo. Anold Kayanda na ripoti kamili.

Akifungua mkutano huo wa wiki mbili aliouita kuwa ni kusanyiko la mataifa yaliyokumbwa na dhoruba za mabadiliko ya tabianchi, Guterres amesema ziara zake Msumbiji, visiwa vya Pasifiki na hata huko Sahel zimedhihirisha kuwa ni lazima hatua zichukuliwe kulindana kuhifadhi mazingira.

Amesema ni lazima dola biliono 100 zipatikane kila mwaka kusaidia nchi zinazoendelea kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kwamba mkutano huo ukubaliane kuhusu ibara ya 6 ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Ibara hiyo ni ile inayohusu mfumo wa masoko ambao unazikubalia nchi kutimiza sehemu ya malengo yake ya ndani kupitia uuzaji wa hewa ya ukaa  ambapo mataifa yanakubaliwa kuuza sehemu yake ya utoaji wa hewa chafuzi, hoja ambayo inaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa,  UNEP, Bi Inger Anderson..

“Tunatambua kuwa kuna maoni tofauti lakini sasa ni wakati kufunga hiyo ibara, kuondoa mabano na kutafuta suluhisho ambalo linaweza kuunganisha kila mmoja pamoja.”

Akisisitiza zaidi kuhusu umuhimu wa ibara hiyo ya sita ya mkataba wa Paris, Mkurugenzi huyo Mkuu wa UNEP anasema,

“Hatuna muda. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliitisha mkutano wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi mwezi Septemba na tulichoikiona pale ilikuwa nchi nyingi kujitokeza na kuongeza matarajio yao, hiyo ilikuwa vizuri, sasa tunahitaji hatua zaidi kufikia makubaliano katika ibara ya sita na kusonga mbele na matarajio na ahadi zaidi za kudhibiti hewa chafuzi.”

Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi ingawa hauzifungi kisheria na wala hauziambii nchi jinsi zinavyopaswa kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi ili kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, lakini unazihimiza nchi kueleza ni nini wanaahidi kufanya, na ni kiasi gani wanapanga kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Anold Kayanda
Audio Duration
2'4"
Photo Credit
UNFCCC