Licha ya wimbi la wakimbizi, bado nchi zilijitoa kimasomaso kuwapatia huduma za afya- UNHCR

18 Julai 2019

Licha ya viwango vya juu vya ukimbizi na hamahama duniani, bado takribani wakimbizi milioni 10.5 walipatiwa huduma ya afya kupitia miradi ya afya kwa umma na mipango ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Takwimu hizo za ripoti hiyo ya takwimu za afya ya umma duniani ya UNHCR zinatokana na utafiti kutoka mataifa 51 yanayohifadhi wakimbizi ambapo maeneo yaliyoangaziwa ni hali ya afya, lishe, maji, huduma za kujisafi na usafi kwa wakimbizi, wasaka hifadhi na jamii zinazowahifadhi.

Kamishna Msaidizi wa  UNHCR anayehusika na operesheni, George Okoth-Obbo amesema wakati asilimia 84 ya wakimbizi wote wanahifadhiwa katika nchi zinazoendelea, ambako huduma za  msingi tayari zimezidiwa uwezo, mifumo ya afya ya kitaifa inahitaji usaidizi ili kuhakikisha wakimbizi na wenyeji wao wanapata huduma muhimu za kuokoa maisha yao.

Ingawa hivyo ripoti imetaja mafanikio  yaliyopatikana kutokana na huduma hizo  kuwa ni pamoja na kupungua kwa viwango vya vifo vya watoto wakimbizi wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Kiwango hicho kimepungua licha ya ongezeko la wimbi la wakimbizi kutoka Myanmar, Sudan Kusin na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Halikadhalika, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya wakimbizi kujumuishwa kwenye mifumo ya matibabu ya kitaifa huku nchi nyingine zikichukua hatua kujumuisha wakimbizi kwenye mifumo ya bima ya afya na hifadhi ya  jamii.

Hata hivyo ripoti inasema bado kuna maeneo yenye pengo kama vile kudhibiti magonjwa ya milipuko miongoni mwa wakimbizi ikitaja milipuko kama vile ugonjwa wa dondakoo na surua Bangladesh na kipindupindu nchini Uganda.

Kwa mantiki hiyo, shirika hilo linasema kwa kuzingatia mwenendo wa ukimbizi unavyozidi kushamiri duniani, UNHCR inahitaji msaada zaidi kwa huduma zake za afya.

Hadi katikati ya mwaka huu wa 2019, UNHCR imepokea asilimia 30 tu ya bajeti ya dola bilioni 8.6 ya kusaidia huduma za kuokoa maisha kwa wakimbizi walioko kwenye mataifa 131.

 

Audio Credit:
Assumpta Massoi/Grace Kaneiya
Audio Duration:
2'11"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud