Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mandela kuenziwa leo kwenye UN; Azimio maalum kupitishwa

Mandela kuenziwa leo kwenye UN; Azimio maalum kupitishwa

Pakua

Leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanapitisha azimio la kumuenzi aliyekuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela.

Hayati Mandela angalikuwa hai mwaka huu, angalikuwa anatimiza umri wa miaka 100 tangu kuzaliwa kwake.

Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imezungumza na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Modest Mero na kumuuliza kiini hasa cha nchi wanachama kuamua kupitisha azimio hilo kuhusu Mandela ambapo amesema.

(Sauti ya balozi Mero)

“Kwasababu Nelson Mandela alitenda mambo mengi ya ajabu, ambayo yamesababisha watu wengi dunia nzima kuyapenda, na hata alifungwa miaka 27 jela sababu kubwa ya kufungwa akiwa anatetea maslahi ya haki ya waafrika kusini. Aliamini kwamba waafrika kusini weusi wana haki sawa na wale wazungu ambao ni wachache”

Ikumbukwe kwamba Afrika kusini ilikuwa imepitisha sheria ya kuwabagua watu weusi ambapo mwaka 1959 Mandela aligomea sheria hiyo ya kibaguzi na aliendelea na msimamo wake huo hata lipokuwa gerezani kisiwani Robben ambapo Balozi Mero amesema.

(Sauti ya balozi Mero)

“Siku zote walipokuwa wamemfunga jela walikuwa wanamuuliza kama amekana yale maneno yake ya kuigomea sera ya kibaguzi. Alikataa kuyakana na mpaka baada ya miaka 27 wakagundua kwamba kwa kweli anachokisema dunia nzima inakikubali na jumuiya ya kimataifa iliamua kupiga vita ubaguzi wa rangi Afrika kusini kwa maandamano kila mahali duniani hatimaye wale wabaguzi wakagundua hawana tena ushirikiano wanaouhitaji na ndiyo maana huu mkutano unazungumzia suala zima la kumuenzi Mandela katika haki za Binamu.”

Inaelezwa pia kuwa jambo lingine ambalo liliuvutia ulimwengu na kumpa sifa kubwa Mzee Nelson Mandela ni pamoja na alivyoamua kuwasamehe wale waliomsweka gerezani na akasema kuwa wajenge taifa moja lisilobagua rangi.

(Sauti ya balozi Mero)

 “Na kwa hivyo basi, kitendo hicho kimeifurahisha Dunia kwamba hata kama umekuwa na mateso makubwa katika kutetea haki za binadamu, unatakiwa kusamehe.” 

Kuhusu yaliyoazimiwa kwenye azimio lenyewe la kumuenzi Mzee Nelson Mandela, Balozi Mero anasema.

(Sauti ya balozi Mero)

“Ni kuhusu haki za msingi za binadamu, suala zima la amani duniani na kutatua migogoro yote iliyopo duniani kwa kutumia njia za amani na vile vile kutowaadhibu watu kwa sababu ya misimamo yao ya kutaka amani. “Amani na maendeleo endelevu pamoja na kutokuwepo migogoro katika nchi ndiyo inayoweza kufanya wananchi wakaendelea. Na hii yote ni misingi ya Umoja wa Mataifa. Kwa Afrika azimio hili linazifundisha nchi na watawala wake kuweza kutatua migogoro yao kwa amani na kuepuka migogoro ambayo siyo ya lazima.” 

Mandela alifariki akiwa na miaka 95 huko Johannesburg Afrika Kusini na kabla ya hapo aliwahi kushinda tuzo ya amani ya Nobel, na kutambulika kama rais aliyeheshimika sana.

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
3'22"
Photo Credit
United Nations Postal Administration (UNPA)