Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na AU sasa bega kwa bega!

UN na AU sasa bega kwa bega!

Pakua

Ziara hii ya pamoja ni utekelezaji wa mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat wa kutaka pande mbili hizo zishirikiane katika kufanikisha ajenda zao za amani na maendeleo.

Viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU wako ziarani Sudan kwa lengo la kuangalia utendaji wa UNAMID, ambao ni ujumbe wa pamoja wa pande mbili hizo jimboni Darfur.

Viongozi hao Jean-Pierre Lacroix ambaye ni mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na Balozi Smail Chergui ambaye ni Kamishna wa amani na usalama wa AU wanaangalia pia mfumo mpya pendekezwa wa UNAMID pamoja na changamoto zinazokumba ujumbe huo katika kutekeleza majukumu yake.

Katika kufanikisha hilo tayari wameshiriki mkutano wa utatu wa AU, Umoja wa Mataifa na serikali ya Sudan, kikiwa ni kikao cha 25 kinachoratibu utendaji wa UNAMID.
Halikadhalika wamekuwa na mazungumzo na pande mbalimbali nchini Sudan kuhusu hali ilivyo huko Darfur.

Baada ya ziara yao huko Sudan, siku ya Jumanne tarehe 10 Bwana Lacroix na Balozi Chergui wataelekea Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambako watajidili ushirikiano kati ya AU na UN katika kusaka suluhu ya kudumu ya kisiasa kwenye mzozo unaoendelea nchini humo.

Wawili hao wataongoza mkutano wa kwanza wa kundi la kimataifa la usaidizi kwa CAR kwa lengo la kushawishi jamii ya kimataifa ijihusishe tena na mchakato wa amani na kusaidia mahitaji ya dharura ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu nchini humo.

Hatimaye Bwana Lacroix na Balozi Chergui wataelekea Addis Ababa Ethiopia ambako tarehe 13 mwezi huu watazungumza kwenye kikao cha Baraza la Amani na Usalama la AU na kukutana na viongozi waandamizi wa chombo hicho.

Ziara hii ya pamoja ni utekelezaji wa mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat wa kutaka pande mbili hizo zishirikiane katika kufanikisha ajenda zao za amani na maendeleo.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'1"
Photo Credit
Ashraf Eissa/UNAMID