Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wachunguzi wa haki za binadamu wataka kuongezwa kwa vikwazo vya silaha Sudan - UN

Wachunguzi wa haki za binadamu wataka kuongezwa kwa vikwazo vya silaha Sudan - UN

Pakua

Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa  wa kutafuta ukweli nchini Sudan, leo Septemba 6 jijini Geneva, Uswisi, wametoa wito wa kuwekwa vikwazo vya silaha kote nchini Sudan kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kikatili kama vile mashambulizi ya kutisha ya kingono.  

Ni mbobevu wa sheria duniani, Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa Ujumbe huo Huru wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Mataifa wa kutafuta ukweli kuhusu yanayoendelea Sudan akiwaeleza waaandishi wa habari leo kwamba, "tangu katikati ya Aprili mwaka 2023, mzozo wa Sudan umeenea hadi majimbo 14 kati ya 18 na kuathiri nchi nzima na ukanda huo, na kuwafanya Wasudan milioni nane kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mzozo huo, na milioni mbili - zaidi ya milioni mbili – kulazimishwa kukimbilia nchi jirani.”

Katika ripoti yao hii ya kwanza tangu Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilipounda jopo hilo mwaka jana 2023, wajumbe hawa wamesisitiza kwamba pande zote mbili zinazohasimiana yaani wanajeshi wa Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), pamoja na washirika wao, wanahusika na mashambulizi makubwa, ya kiholela na ya moja kwa moja yaliyohusisha mashambulizi ya anga na makombora dhidi ya raia, shule, hospitali, mitandao ya mawasiliano na miundombinu mingine muhimu ya maji na umeme ikionesha kutozingatia kabisa ulinzi wa wasio wapiganaji.

Joy Ngozi Ezeilo, mmoja wa wajumbe wa jopo hilo la wataalamu huru anaeleza kwamba, waathirika walisimulia kushambuliwa wakiwa kwenye nyumba zao na kutishiwa kifo au kuumizwa kwa ndugu au watoto wao kabla ya kubakwa na zaidi ya mtu mmoja.”

Wachunguzi hao licha ya kupendekeza uwekaji zaidi wa vikwazo vya silaha kwa Sudan, pia wamehimiza kuanzishwa kwa kikosi cha kimataifa cha kulinda amani na ama kiwe chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa au mamlaka nyingine ya kikanda.

Audio Credit
Cecily Kariuku
Sauti
1'54"
Photo Credit
© UNICEF/Mohamed Zakaria