Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wa asili wana haki ya kulinda utamaduni wao: Guterres

Watu wa asili wana haki ya kulinda utamaduni wao: Guterres

Watu wa jamii ya asili wasilazimishwe kuishi maisha yasiyo asili yao – Guterres
 
Kulinda haki za watu wa jamii ya asili za kujitenga kwa ridhaa na kuishi maeneo yao asili ndio ujumbe wa mwaka huu wa siku ya kimataifa ya watu wa jamii ya asili dunia, ujumbe ambao Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni sahihi na kila mtu anapaswa kuuzingatia.
 
Kupitia ujumbe wake wa video kwa siku hii, Guterres anasema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa,
 
(Sauti  ya Antonio Guterres) Bosco
 
“Watu wa jamii ya asili ni asilimia 6 ya wakazi wote duniani. Lakini jukumu walilobeba ni mchango mkubwa kwa jamii yetu ya dunia. Wanahifadhi ufahamu na tamaduni zinazosaidia kulinda baadhi ya bayonuai muhimu zaidi za sayari yetu. Kama walinzi wa mazingira, uhai wao ndio uhai wetu.”
 
Ingawa hivyo anasema wanakabiliwa na changamoto kubwa la tishio la uwepo wa kwani mara nyingi ni manusura wa vitisho na ghasia.
 
(Sauti ya Antonio Guterres) Bosco
 
“Sekta za uziduaji na uzalishaji kama vile madini, kilimo na usafirishaji zimechochea ukataji miti na mmomonyoko wa udongo. Makazi ya mababu na maliasili ambazo wanategemea zimevamiwa. Huku haki zao za kujitawala zilizomo kwenye Azimio la Umoja wa Mataifa la watu wa asili bado hazijatekelezwa.”
 
Changamoto nyingine ni magonjwa ya maambukizi, kulazimishwa kuiga tamaduni zingine na kuvurugwa kwa tamaduni, lugha na mbinu zao za kuishi.
 
Guterres anasema ujumbe wa mwaka huu unakumbusha umuhimu wa kulinda haki za watu wa asili za kujilinda dhidi ya utangamano usio wa lazima, utangamano ambao amesema unaweza kuwa na madhara makubwa.
 
Leo na kila siku, dunia ishikamane na haki za watu wa asili ili wasongeshe mustakabali wao. Kwa pmoja, amesema Guterres hebu na tulinde haki zao za kuishi kwa amani na utu.

Pakua
Audio Credit
UN News/ Flora Nducha
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
UNHCR Video