Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu yatanda mzozo Mashariki ya Kati kusambaa zaidi

Hofu yatanda mzozo Mashariki ya Kati kusambaa zaidi

Pakua

Kamishina Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za binadamu Volker Türk leo ameonya juu ya ongezeko la hatari ya kusambaa kwa mzozo Mashariki ya Kati na kuzitaka pande zote husika kutoa kipaumbele cha kuwalinda raia. Flora Nducha na taarifa zaidi

Asante Assumpta. Katika taarifa yake fupi iliyotolewa mjini Geneva Uswis  Kamishina Mkuu Türk amesema “Nina wasiwasi mkubwa juu ya hatari inayoongezeka ya mzozo mkubwa zaidi Mashariki ya Kati na ninazisihi pande zote husika katika mzozo huu, pamoja na nchi zenye ushawishi, kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti hali hii ambayo imekuwa ni ya hatari sana.”

Amesisitiza kuwa kwa hali yoyote ile “Haki za binadamu  na hasa ulinzi wa raia lazima iwe kipaumbele cha kwanza.”

Kamishina Mkuu huyo wa Haki za binadamu amesema tayari, katika kipindi cha miezi 10 iliyopita ya mzozo huo, raia wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamevumilia madhila na mateso yasiyoweza kuvumilika kutokana na mabomu na mtutu wa bunduki unaorindima kila uchao.

Hivyo amesema “Kila kitu, na ninamaanisha kila kitu, lazima kifanyike ili kuepusha hali hii kusambaa zaidi na kutumbukia kwenye shimo ambalo litakuwa na matokeo mabaya zaidi kwa raia.”

Tangu mzozo huo kuanza Oktoba 7 mwaka jana shirika la Umoja  wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa  Kipalestina UNRWA limesema zaidi ya watu 38,000 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 88,000 kujeruhiwa huku mateka zaidi ya 110 bado wanashikiliwa.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Sauti
1'35"
Photo Credit
© UNRWA