Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asanteni watu wa White Nile kuwapokea wakimbizi wa ndani kutoka Blue Nile - Khardiata Lo N’Diaye

 Wakimbizi wa Sudan kutoka jimbo la Blue Nile, wanaoishi katika kambi ya Doro katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini
Photo UNHCR/V. Tan
Wakimbizi wa Sudan kutoka jimbo la Blue Nile, wanaoishi katika kambi ya Doro katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini

Asanteni watu wa White Nile kuwapokea wakimbizi wa ndani kutoka Blue Nile - Khardiata Lo N’Diaye

Wahamiaji na Wakimbizi

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu nchini Sudan, Khardiata Lo N’Diaye hii leo akizungumzia kuhusu kuhamishwa kwa wakimbizi wa ndani (IDPs) kuelekea Jimbo la White Nile ametoa shukrani kwa serikali ya Jimbo la White Nile na “muhimu zaidi, jumuiya za Kosti na Rabak. Wametoa makazi na usaidizi unaohitajika kwa watu hawa waliofurushwa, zaidi ya watu 19,000 kati yao waliishi katika White Nile.”

Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya OCHA mjini Khartoum, Sudan, Khardiata Lo N’Diaye amesema, kufuatia matukio ya Julai 2022, awali alishaeleza wasiwasi mkubwa juu ya makumi ya raia waliouawa na maelfu ya wanawake na watoto waliokimbia vurugu kati ya jamii moja na nyingine huko Ar Rusayris, Damazine, na maeneo mengine ya Jimbo la Blue Nile.  

Mtoto nchini Sudaa akipokea lishe ya karanga kwa ajili ya matibabu ya utapiamlo
© UNICEF/Shehzad Noorani
Mtoto nchini Sudaa akipokea lishe ya karanga kwa ajili ya matibabu ya utapiamlo

Nina mashaka bado 

Pamoja na kwamba wakimbizi wamepata pa kuhifadhiwa, lakini kiongozi huyo anasema bado ana mashaka, akisema, “wengi wa wakimbizi hawa wa ndani (IDPs) waliweza kuhifadhiwa ndani ya jamii za White Nile. Hata hivyo, ninabaki na wasiwasi mkubwa kuhusu jinsi uhamisho huu ulivyofanyika. 

Bi. Lo N’Diaye amesema ni wajibu wa nchi kuzuia kufurushwa, kuwalinda na kuwasaidia watu waliofurushwa kutoka katika makazi yao na kutambua suluhu za kudumu kwao, “ninatoa wito kwa mamlaka za Jimbo kuendelea kutoa ufikiaji wa huduma muhimu, makazi, huduma za afya, elimu, kipato na kadhalika ndani ya jamii wenyeji, kuhakikisha uhuru wa kutembea na ulinzi kwa wakimbizi wa ndani waliofurushwa.” 

“Ingawa ninapongeza majaribio ya mamlaka ya Serikali kupata eneo la kuwahamishia huko Khor Ajwal, ni muhimu kwamba kuhamishiwa katika maeneo kama hayo ni kwa hiari na kwamba washirika wa kibinadamu wanaweza mapema kutathmini kufaa kwa maeneo hayo na usalama.” Amesema. 

Aidha ameeleza kuwa uamuzi wa mamlaka ya Jimbo kusitisha kwa muda ufurushaji wa wakimbizi wa ndani mnamo tarehe 5 Oktoba 2022 ili kuruhusu watendaji wa kibinadamu kuanzisha kiwango fulani cha huduma za kimsingi ni ishara chanya na akatoa wito kwa mamlaka za Serikali kuendelea kuwawezesha wahusika wa kibinadamu wasio na vikwazo kuruhusu watendaji wote wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa, na NGOs za kimataifa na za kitaifa, kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu hawa wanaohitaji.

“Ninawasihi wahusika wa masuala ya kibinadamu kuendelea kujihusisha kwa njia yenye kujenga na kuthamini usaidizi wa ziada unaotolewa ili kukabiliana na upungufu wa chakula na makazi.” Ametoa ombi Bi. Lo N’Diaye. 

Watendewe kibinadamu 

Mwisho kiongozi huyo amehimiza mamlaka za Serikali nchini Sudan kuwatendea watu waliohamishwa makazi yao kulingana na kanuni, viwango na kanuni za kibinadamu.

Nawaomba wadau wote waendelee kushughulikia vyanzo vya migogoro hiyo na kuweka mazingira yatakayowawezesha watu hao kurejea majumbani mwao kwa hiari na kuhakikishiwa usalama wao wa muda mrefu. Jumuiya ya misaada ya kibinadamu iko tayari kutoa msaada wa kibinadamu kwa wale walioathirika na kufanya kazi na mamlaka ili kupata suluhisho endelevu kwa watu wote waliokimbia makazi yao nchini Sudan.”