Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 5 tu baada ya uhuru wa Tanzania bara, tulijiunga Umoja wa Mataifa na pande zote zinanufaika - Songelael Shilla

Kaimu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Songelael Shilla
Assumpta Massoi
Kaimu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Songelael Shilla

Siku 5 tu baada ya uhuru wa Tanzania bara, tulijiunga Umoja wa Mataifa na pande zote zinanufaika - Songelael Shilla

Amani na Usalama

Siku kama ya leo tarehe 9 mwezi Desemba mwaka 1961, iliyokuwa Tanganyika au Tanzania Bara ilipata Uhuru wake kupitia mchakato uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Siku 5 baadaye, nchi hiyo huru ilijiunga na Umoja wa Mataifa na kuwa mwanachama hadi leo na hii leo inaposherehekea miaka 60 ya uhuru wake, pia inatambua faida inazozipata kwa kuwa mwanachama wa UN kama anavyoeleza Kaimu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Songelael Shilla alipozungumza na Idhaa hii jijini New York Marekani.

"kwanza mchakato wote wa kuapata uhuru umefanyika katika mazingira hayo ya Umoja wa Mataifa. Na kutokea hapo Tanzania imeendelea kuwa mjumbe mwaminifu sana tukichangia mengi lakini pia tukinufaika mengi kwa kuwa wanachama wa Umoja wa Mataifa. Tuna mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo yapo nchini mwetu yakishughulika na shughuli za maendeleo, miradi mbalimbali ya maendeleo, ya afya, ya elimu na vitu kama hivyo, mambo ambayo tusingeyapata kama tusingekuwa wanachama."

Pamoja na Tanzania kunufaika na Umoja wa Mataifa, nayo pia imekuwa na mchango mkubwa kwa ulimwengu kama anavyofafanua Bwana Shilla,"dunia imenufaika sana na Tanzania kupitia Umoja wa Mataifa kwa sababu Tanzania imekuwa ni nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele sana kwenye usuluhishi wa migogoro mbalimbali ya kisiasa, imekuwa mstari wa mbele sana kwa maana kwama kwenye maeneo yetu ukanda wa maziwa makuu, Jumuiya ya SADC, Afrika Mashariki, kote Tanzania imeshiriki kwa kiasi kikubwa kusuluhisha migogoro ambayo ilikuwa inatokea kwenye ukanda wetu na kwa maana hiyo Umoja wa Mataifa umekuwa ukiitegemea sana Tanzania kuwa ni msaidizi wa Umoja wa Mataifa katika usuluhishi wa migogoro. Lakini kwa upande mwingine Tanzania inachangia vikosi vya askari na watumishi raia kwenye misheni za ulinzi wa amani karibu sita za Umoja wa Mataifa ambako huo ni mchango mkubwa kwa sababu tunajitolea maisha ya watu kwenda kulinda amani kwenye nchi ambazo zina matatizo ya amani, zima migogoro, vita na vitu kama hivyo. Kitu ambacho ni mchango mkubwa kwa kiasi kwamba huwezi hata ukaulinganisha kifedha."