Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati za Baraza Kuu zaanza kujadilia ajenda za kikao cha 62

Kamati za Baraza Kuu zaanza kujadilia ajenda za kikao cha 62

Baraza Kuu la UM lina kamati sita ambazo zimegaiwa majukumu kadha wa kadha yanayohusiana na masuala ya kimataifa yenye kuhitajia suluhu ya kipamoja miongoni mwa jamii ya kimataifa.

Kamati ya Pili ya Baraza Kuu huzingatia mada zinazoambatana zaidi na masuala ya Fedha na Uchumi, na mwaka huu Kamati imefungua mijadala yake kwa kushauriana taratibu zinazofaa kuchukuliwa kukabiliana na matatizo yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, na vile vile kubadilishana mawazo juu ye utekelezaji wa dharura way ale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na pia huduma za kudumisha maendeleo.

Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu huzungumzia masuala ya kiutu na kijamii, na wajumbe wa kamati sasa hivi wanafanya mapitio juu ya ripoti zinazoambatana na namna haki za binadamu zinavyotekelezwa katika Nepal, na vile vile katika Uganda.

Kamati ya Nne inajadilia mada anuai za kisiasa, hususan yale masuala ambayo huwa hayajapata fursa ya kushughulikiwa na Kamati ya Kwanza. Kadhalika Kamati hii imepewa dhamana ya kuzingatia, kwa ukamilifu, masuala maalumu yanayoambatana na juhudi za kukomesha ukoloni duniani pote.

Kamati ya Tano inazungumzia masuala ya utawala wa kazi katika UM pamoja na bajeti la kuendesha shughuli za taasisi hii ya kimataifa.

Na Kamati ya mwisho ya Baraza Kuu la UM ni ile Kamati ya Sita ambayo kazi zake hasa hulenga zaidi kwenye masuala yanayofungamana na sheria ya kimataifa. Mapema wiki hii Kamati imeanza kutathminia namna UM unavyotetea haki kazi za watumishi wake.