Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Elimu Duliani 2024 yatumika kukabiliana na kauli za chuki

Siku ya Elimu Duliani 2024 yatumika kukabiliana na kauli za chuki

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeyatumia maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Elimu kuangazia jukumu muhimu la elimu na walimu katika kukabiliana na kauli za chuki, jambo ambalo limekithiri katika miaka ya hivi karibuni kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii na hivyo kuharibu muundo wa jamii kote duniani. 

UNESCO ambalo ndilo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika moja kwa moja na jukumu la kuratibu maadhimisho ya siku hii ya kimataifa ya elimu inayodhimishwa kila mwaka tarehe 24 Januari, linasema ulimwengu unashuhudia ongezeko la migogoro inayoambatana na ongezeko la kutisha la ubaguzi, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, na kauli za chuki. Na kwa kuwa madhara yanavuka mipaka yoyote ya kijiografia, jinsia, rangi, dini, siasa, nje ya mtandao na mtandaoni elimu ni msingi wa kufanikisha kupambana na hali hiyo.

Audrey Azoulay ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO kupitia ujumbe wake mahususi kwa siku hii akifafanua kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni ‘Elimu kwa ajili ya amani ya kudumu’ amesema, “kwa sababu kama chuki inaanza kwa maneno, basi amani inaanza na elimu. Tunachojifunza hubadilisha jinsi tunavyouona ulimwengu na huathiri jinsi tunavyowatendea wengine. Kwa hivyo elimu lazima iwe kiini cha juhudi zetu za kufikia na kudumisha amani ya ulimwengu.” Anasisitiza kwamba, katika siku hii, kujitolea kwako kutetea haki ya elimu bora ambayo inatambua haki za binadamu za kila mtu inamaanisha kujitolea kwa mustakabali wa amani kwa wote, ambapo kila mtu anaweza kuishi maisha ya utu, kwa kuelewana na heshima.

Ili mawazo haya yawafikie watu wengi zaidi ulimwenguni, UNESCO hii leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani imewakutanisha wadau wa elimu kutoka kote ulimwenguni ili kujadili mchango muhimu wa elimu katika kufikia amani endelevu duniani. Pia imefanya mafunzo ya mtandaoni ya siku moja kwa maelfu ya walimu kutoka kote ulimwenguni kuhusu utatuzi wa kauli za chuki, ambayo yamewapa zana za kutambua vyema, kukabiliana na kuzuia matukio ya kauli za chuki. Mafunzo haya ni sehemu ya hatua ya UNESCO kusaidia Nchi Wanachama na wataalamu wake wa elimu kushughulikia kauli za chuki kupitia elimu.

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
2'10"
Photo Credit
© UNICEF/Milequem Diarassouba