Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yasema inashikamana na Japan wakati huu taifa hilo limekumbwa na tetemeko kubwa la ardhi

UN yasema inashikamana na Japan wakati huu taifa hilo limekumbwa na tetemeko kubwa la ardhi

Pakua

Harakati zikiendelea za kunasua watu waliokwama kwenye vifusi kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililokumba eneo la kati mwa Japan Jumatatu alasiri kwa saa za huko na kusababisha vifo vya watu 62, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake kufuatia tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Richa. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Florencia Soto Nino aliwaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kwamba, “Katibu mkuu amehuzunishwa sana na taarifa za vifo na uharibifu wa mali uliosababishwa na tetemeko. Na ameelezea mshikamano wake na serikali ya Japan na watu wa Japan. Ametuma pia salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kutakia ahueni ya haraka majeruhi.” 

Vyombo vya  habari vinaripoti ya kuwa zaidi ya waokoaji 3,000 wamefika eneo la tukio ambalo ni katikati mwa Japan kwa ajili ya kunasua watu waliokwama kwenye vifusi huku moto ukiripotiwa kulipuka kwenye eneo hilo. 

Kitovu cha tetemeko hilo ni rasi ya Noto, katikati mwa Honshu ambacho ndio kisiwa kikubwa nchini Japan kinachojumuisha maeneo kama vile Tokyo, Kyoto, Osaka na Hiroshima. Bi. Soto Nino amezungumzia pia ajali ya ndege ya shirika la ndege la Japan na ndege iliyokuwa inaelekea kutoa msaada eneo la tetemeko la ardhi ambapo abiria wote kwenye ndege walinusurika ilhali wafanyakazi watano wa ndege ya misaada wamepoteza maisha. 

“Mawazo yetu kwa sasa yako na wananchi wa Japan na tunatumai kuwa wataweza kujikwamua kwenye hili.” 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Sauti
1'36"
Photo Credit
© IMF