Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR linasema mashtaka yote dhidi ya waokoaji wa wahamiaji baharini huko Ugiriki yafutwe

OHCHR linasema mashtaka yote dhidi ya waokoaji wa wahamiaji baharini huko Ugiriki yafutwe

Pakua

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu kesi iliyoanza huko Lesvos nchini Ugiriki dhidi ya watetezi 24 wa haki za binadamu wanaoshtakiwa kwa kutekeleza jukumu la kuokoa wahamiaji ambao walikumbwa na zahma baharini wakati wakikimbilia barani Ulaya kusaka maisha bora.

Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Liz Throsell amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa kesi za namna hiyo zinaharamisha kazi zinazookoa maisha na kuweka mwelekeo wa hatari. 

Msemaji huyo amesema anatambua kuwa leo asubuhi mwendesha mashtaka huko Mytilini mjini Lesvoc kunakofanyika kesi hiyo amependekeza kufutwa kwa baadhi ya mashtaka na hivyo amesema, “tutakaribisha maendeleo kama hayo, lakini tunasisitiza kuwa mashtaka yote dhidi ya watetezi hao wa haki za binadamu yafutwe.” 

Bi. Throsell amesema tayari kumekuweko na hofu ambapo watetezi wa haki za binadamu na mashirika ya kiutu huko Ugiriki na katika nchi wanachama wa Muungano wa Ulaya wamelazimika kusitisha kazi zao za haki za kiutu kutokana na hofu. 

Ametoa wito kwa mashtaka dhidi ya watetezi hao wote 24 wa haki za binadamu yatupiliwe mbali akisema, mashtaka yao yanahusiana na vitendo vyao vya kuokoa wahamiaji baharini na madai ya tabia mbayá ya kwamba wanafanikisha usafirishaji haramu wa wahamiaji, 

Amesisitiza kuwa kuokoa maisha na kutoa msaada wa kibinadamu katu hakupaswi kuharamishwa na kwamba vitendo hivyo vya usaidizi badala yake ni vya kiutu na vinakubalika. 

Wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wanachama au wafanyakazi wa kujitolea katika shirika la kiraia la kimataifa la uokaji nchini Ugiriki, ERCI, shirika ambalo tangu mwaka 2016 hadi 2018 limesaidia zaidi ya watu 1,000 kufika eneo salama. Halikadhalika limepatia manusura huduma za matibabu na misaada mingine. 

Tangu kukamatwa kwa watetezi hao, shirika hilo limelazimika kufunga operesheni zake ilhali watetezi wamekuwa wakisubiria kuanza kwa kesi yao kwa miaka minne hadi ilivyoanza wiki hii. 

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'12"
Photo Credit
IOM 2016/Amanda Nero