Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika kuhakikisha uhakika wa chakula: FAO

Sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika kuhakikisha uhakika wa chakula: FAO

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya uvuvi duniani imeelezwa kuwa sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika kuhakikisha uhakika wa chakula na inasaidia mtu 1 kati ya 10 duniani kote. Kwa kutambua mchango wake wito umetolewa na Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO kuboresha miasha ya mamilioni ya wanawake kwa wanaume wanaofanyakazi katika sekta hii kwa kuhakikisha haki zao za binadamu zinatimizwa.  

Kupitia ujumbe wake wa siku hii mkurugenzi mkuu wa FAO Dkt. QU Dongyu, amesema kwa muda mrefu FAO imekuwa ikiwasaidia mamilioni ya wanawake na wanaume wanaofanyakazi katika sekta ya uvuvi na watu wa jamii za asili kote duniani kwa sababu ni sekta muhimu katika mfumo wa chakula na mnyororo wa thamani  ambayo inatoa fursa kubwa ya ajira hususan kwa nchi zinazoendelea. 

Pia inasaidia kujenga jamii imara za watu wa Pwani na kuhakikisha uhakika wa chakula la lishe kwa mamilioni ya watu. 

 Bwana Dongyou ameongeza kuwa “Samaki na bidhaa za Samaki ni miongoni mwa bidhaa za chakula zinazouzwa sana duniani kote na mwaka 2019 pekee iliingiza takriban dola bilioni 163 za mapato ya usafirishaji nje huku nchi zilizoendelea zikiongeza kiwango chake cha thamani ya biashara ya kimataifa ya bidhaa za Samaki kwa zaidi ya asilimia 54.” 

Mkuu huyo wa FAO amesema pamoja na mchango huo mkubwa kwa lishe na maendeleo “Kwa bahati mbaya sekta hiyo inayotoa fursa kubwa kwa wavuvi na wafanyakazi wa uvuvi inaweza pia kuwaathiri  wasiojiweza kupitia ukiukwaji wa haki za wafanyakazi ambazo zinajumuisha mfumo usio wazi wa ajira ambao hauhakikishi malipo bora kwa wafanyakazi, kufanyakazi kwa saa nyingi zisizoendana na malipo, ajira ya shuruti, ajira kwa watoto na mambo mengine.” 

 Kwa mantiki hiyo Dongyou amesisitiza “Tunahitaji kuwapa sauti wanafanyakazi ha wa na kushikamana nao katika vita vya kuwa na ajira yenye staha kwa kupitia kuongeza ushirikiano miongoni mwa wadau wote zikiwemo nchi, mashirika ya kimataifa, vyama au jumuiya za wavuvi, sekta binafsi, jumuiya za wafanyakazi, mashirika ya asasi za kiraia na walaji.” 

Pamoja na mikataba mingine iliyopo FAO imesema inazindua mwongozi mpya kuhusu wajibu wa kijamii kwa makampuni yaliyoko kwenye sekta ya uvuvi na pia itaendelea kusfanyakazi kwa karibu na wadau wengine kama shirika la kazi la Umoja wa Mataifa duniani ILO kusaidia kuboresha mazingira ya kazi na maisha ya jamii za wavuvi kote duniani ikiwemo haki zao za masingi za binadamu. 

Siku ya uvuvi duniani huadhimishwa kila mwaka Novemba 21 na mwaka huu imebeba maudhui "Kuzuia wimbi: Kwa pamoja tunaweza kukomesha ukiukaji wa haki za binadamu baharini!". 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration
2'58"
Photo Credit
Unsplash/Roberto Carlos Roman Don