Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hewa chafu ni tishio kwetu sote

Hewa chafu ni tishio kwetu sote

Pakua

Asilimia 90 ya wakazi wa dunia huvuta hewa chafu na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya duniani, WHO  iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo inasema uvutaji huo wa hewa hiyo umesababisha watu zaidi ya milioni 7 kufariki dunia kila mwaka kutokana na chembechembe wanazopata wakivuta hewa chafu.

WHO inasema chembechembe  za hewa chafu zinapoingia katika mapafu au moyo huweza kusababisha magonjwa  kama vile moyo na pumu.

Ingawa mataifa mengi sasa yanachukua hatua dhidi ya hewa chafu, WHO inasema bado takwimu za vifo ni za juu.

Akitoa kauli kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus, amesema uchafuzi wa hewa ni tishio kwa kila mtu lakini wanaoumia zaidi ni watu maskini.

Amesema haikubaliki kwamba watu billioni tatu na wote ni wanawake na watoto bado wanavuta hewa chafu kila siku inayotoka kwenye majiko wanayotumia majumbani.

 Dkt. Ghebreyesus [GeBreYeSus] ameonya kuwa ikiwa hakutachukuliwa hatua za haraka, kamwe dunia haitaweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya kuhakikisha kila mtu anavuta hewa safi.

Mkuu huyo wa WHO amesema ni matumaini yake kuwa viongozi mbalimbali wakiwemo mameya wa miji watachukua hatua madhubuti.

Amepongeza serikali ambazo amesema zimeanza kuvalia njuga suala hilo kwa kuweka njia za kupunguza utoaji wa hewa chafu katika maeneo yao.

Tags: Hewa chafu, WHO, SE4All

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
2'4"
Photo Credit
Picha@UNFCCC