Wengi wa wananchi wa Gaza milioni 2.3 wanakimbia ghasia zinazozidi kaskazini na Kusini mwa Gaza kutokana na vita ambayo sasa ina miezi saba na ambayo imesababisha vifo vya wapalestina 36,000 na kuwaacha wengine katika njaa huku wengine wakiwa wamefukiwa kwenye vifusi katika maeneo yaliyo zingirwa.
Wananchi wengi wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa. Wengi wao walisafiri hadi Rafah, kusini mwa Gaza, ambako Israeli ilikuwa imetangaza kuwa ni eneo salama.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA hali katika makazi ya muda huko Rafah zilikuwa mbaya. Watu walikuwa wamejazana ndani ya safu za mahema na majengo ya kubahatisha, wanaume, wanawake na watoto waliokimbia makazi yao walikabiliwa na uhaba wa chakula, maji na mahitaji muhimu ya kila siku.
Hadi kufikia tarehe 20 Mei, zaidi ya asilimia 75 ya Ukanda wa Gaza - takriban kilomita za mraba 285 (maili za mraba 141) - ilikuwa chini ya maagizo ya kutakiwa kuhama huku kukiwa na ongezeko la uhasama, kulingana na taarufa iliyotolewa hivi karibuni na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu wa Misaada ya Kibinadamu, OCHA.
Watu wamekuwa wakihamia maeneo ya katikati mwa Gaza ambayo pia yanashambuliwa na kukosa mahitaji muhimu kama vile chakula na maji. Hali hii huenda ikasababisha kuongezeka kwa magonjwa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na hepatitis A, pamoja na utapiamlo, limesema shirika la OCHA.
Wakimbizi wa kimatibabu kutoka kaskazini mwa Gaza ni pamoja na watoto wengi, mmoja wao ni Ibrahim mwenye umri wa miaka 13, ambaye aliumia sana kufuatia kuporomoka kwa makazi katika eneo lililotengwa na kuelezwa ni salama ambapo alikaa na familia yake. Ibrahim hatimaye alipoteza mkono wake wakati wa kukatwa mguu bila kutumia ganzi.
OCHA imesema watu waliokimbia makazi yao kutoka Rafah kwa sasa wanatafuta hifadhi katika maeneo ya Khan Younis na Deir Al-Balah katikati mwa Gaza kwenye ardhi yoyote ya wazi inayopatikana, ikiwa ni pamoja na barabara za kuingia katika eneo hilo, ardhi ya kilimo na katika majengo yaliyoharibiwa ambayo hayajatathminiwa kimuundo.