
Tarehe 15 mwezi Julai kila mwaka ni siku ya kimataifa ya stadi kwa vijana. Umoja wa Mataifa ulipitisha siku hii mwaka 2014 kama njia ya kuibua mbinu mpya za kuwezesha vijana kupata stadi bora. Umoja wa Mataifa unataka elimu ya darasani iende sambamba na mafunzo ya stadi.
Nchini Lebanon, kijana akichomelea machuma. UNICEF nchini humo imeona inavutia vijana na kupitia mafunzo ya stadi pia wanapatiwa kipato kidogo na hatimaye watajitegemea badala ya kusalia bila ajira yoyote.

Wahenga walinena 'samaki mkunje angali mbichi kwani akikauka hakunjiki,' na ndivyo ilivyo pichani kwa mtoto Natalia kupitia kusaidia bibi yake kuuza genge, naye anapata stadi za kuangia kwenye ujasiriamali. Je wewe unasaidia familia yako?

Ingawa ana ulemavu, Nayeem mwenye umri wa miaka 14 na kutoka Bangladesh, hakukubali hali hiyo ikwamishe ndoto zake. Jirani yao amemfundisha stadi za uhandisi na ameweza kutengeneza tochi yao ambayo ilikuwa imeharibika. Kila mtu ana uwezo wa kujifunza stadi apendayo.

Teknolojia ina nafasi kubwa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu na pichani ni Debora Mtambalika kutoka malawi na anatuonesha drone au ndege isiyo na rubani ambayo ametengeneza wakati anapata mafunzo ADDA ambacho ni chuo cha mafunzo ya utengenezaji wa ndege zisizo na rubani nchini Malawi.