Haiti inasema kwaheri vikosi vya ulinzi wa amani vya UN vilivyodumu nchini humo kwa miaka 15


Walinda amani wa UN wamepelekwa nchini Haiti kwa miaka 15 iliyopita kufuatia kuyumba kwa uatawala wa kishera, na mpango huo unakamilika Oktoba mwaka huu wa 2019. Mwanzoni, mnamo mwaka wa 2005, wanajeshi, polisi na walinda amani raia walihamia kwenye kisiwa hicho cha Karibea kama jukumu lao la kulinda raia na kusaidia kurejesha utawala wa seheria na utulivu.

Moja ya vipaumbele vya walinda amani hao ilikuwa ni kurejesha tena amani na usalama kupitia doria, vituo vya ukaguzi na shughuli za kudhibiti uhalifu. Hapa, wanajeshi wa Brazil wanashika doria sehemu iliyo na shida ya mji mkuu, Port-au-Prince.

Kushirikiana na watu wa eneo hilo ili kuelewa mahitaji yao ilikuwa sehemu muhimu ya kazi ya awali ya vikosi hivyo. Hapa, maafisa wa Polisi wa UN wanazungumza na watoto wakiwa kwenye doria katika mji mkuu.

Mpango wa UN pia ulifanya kazi na jamii kwenye miradi ya kupunguza machafuko. Walinda amani waliunga mkono wafanyikazi hawa wa Haiti, wakiwasaidia kujenga kuta na kupanda miti ili kuhifadhi mazingira na kuzuia mafuriko. Mradi huo pia uliwezesha fursa za kiuchumi na kijamii kwa washiriki wa zamani wa magenge ya uhalifu.

Mpango pia uliunga mkono uchaguzi wa rais, sheria na manispaa katika taifa la kisiwa hicho. Hapa, bibi anasaidiwa kutembea ili afike kwenye kibanda cha kupiga kura mnamo 2006, huko Port-au-Prince, na afisa wa polisi wa Umoja wa Mataifa.

Mpango wenyewe wa kulinda amani ulichukua jukumu muhimu la usafirishaji wa kura kutoka nchi nzima kwenda mji mkuu. Walinda amani pia walilinda usalama wakati upigaji kura ukifanyika.

Haiti imepitia misiba ya asili kwa muda wa miaka 15 hadi sasa. Hapa, mlinda amani wa UN kutoka Brazili amebeba mtoto ambaye aliokolewa kufuatia mafuriko katika kitongoji cha Cité Soleil cha Port-au-Prince.

Mnamo Januari 2010, tetemeko kubwa la ardhi liliikumba Haiti, ambapo watu 220,000 waliripotiwa kupoteza maisha. Jumla ya wafanyikazi wa UN 102 pia walipoteza maisha wakati makao makuu ya mpango wenyewe yalipobomoka.

Maelfu zaidi walijeruhiwa katika tetemeko hilo la sekunde 47 na wengi, kama kijana huyu, walitibiwa na walinda amani wa UN.

Umoja wa Mataifa ulisaidia kuanzisha jeshi lenye nguvu la polisi 15,000 la Haiti. Wanawake wamehudumu kama maafisa wa polisi wa UN nchini humo, pamoja na kitengo hiki cha wanawake kutoka Bangladesh.

Mpango wa sasa wa kulinda amani ya Umoja wa Mataifa unafungwa Oktoba 15, mwaka huu wa 2019 na utabadilishwa na nafasi yake kuchukuliwa na mpango wa kisiasa, ukiendeleza maendeleo ambayo yamefanywa na mamlaka ya Haiti ya kuimarisha utulivu, usalama, utawala, pamoja na sheria na haki za binadamu.