
Katapila hizo za Umoja wa Mataifa zinasaidia kuweka barabara tambarare na hivyo kurahisisha usafiri. Mvua za msimu wa masika ziliharibu barabara na kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyoanza mwezi Desemba mwaka 2013, ukarabati unakuwa haufanyiki mara kwa mara.

Ukarabati wa barabara unaenda sambamba na doria ili kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo hayo wanaendelea na shughuli zao. Wakati wakiwa doria walinda amani kama huyo kutoka alipata fursa pia ya kuzungumza na watoto ambao walikuwa na shauku ya kusikia kutoka kwa mlinda amani huyo kutoka Thailand.

Barabara zinapokuwa nzuri na zinazopitika, hata usafirishaji wa bidhaa muhimu kama vile nishati ya mkaa unakuwa ni rahisi na hata bei nayo kwa mtumiaji inakuwa ni rahisi, kama aonekanavyo mfanyabiashara wa mkaa akiwa na magunia yake akipita wakati ukarabati wa barabara ukiendelea.

Barabara zinapokuwa mbovu na hazipitiki hata usafirishaji wa abiria unakuwa wa shida kwa kuwa ni magari machache yanaweza kuhimili barabara mbovu. Pichani kauli ya "msafiri kafiri" ikiwa inadhihirika kwa kuwa msafiri katika barabara kama hii hawezi kuchagua usafiri, lakini hali hii inatishia usalama wao na ndio maana Umoja wa Mataifa umechukua hatua kukarabati.

Ukarabati ukiendelea sambamba na doria za pamoja za walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Nepal na Thailand, wanafunzi nao wanaorejea nyumbani kutoka shuleni hawana wasiwasi njiani kuhusu usalama wao na wao wanapata fursa ya kubadilishana mawazo na walinda amani hao.