
Hapa ni Mangina jimboni Kivu Kaskazini ambapo kitengo cha tabia na nidhamu cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kimeendesha semina kwa wanafunzi 543 wakiwemo wasichana 263 kutoka taasisi ya AHADI. Semina hii imewahamasisha kuhusu harakati dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kingono unaofanywa na watendaji wa Umoja wa Mataifa na mawakala ikiwa ni utekelezaji wa ajenda ya Umoja wa Mataifa ya kutovumilia kabisa vitendo hivyo vifanywavyo na watendaji wake.

Pichani ni wanawake manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kingono kwenye eneo la Sake jimboni Kivu Kaskazini, wakionyesha uyoga ambao wamevuna ikiwa ni mradi uliosimamiwa na kitengo cha tabia na nidhamu cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Mradi huu unasaidia wanawake hawa kuongeza kipato na ni moja ya miradi kama vile ushonaji na uoakaji mikate inayotekelezwa kwenye eneo hilo.

Sanaa za maonyesho nazo pia zinashamiri kama ionekanavyo pichani ambapo ni mojawapo ya mbinu ya kuhamasisha jamii kuhusu athari za ukatili na unyanyasaji wa kingono unaoweza kufanywa na watendaji wa Umoja wa Mataifa na mawakala wao. Hapa ni Sake mjini Masisi kwenye jimbo la Kivu Kaskazini. Maigizo haya ya sanaa yanapatia jamii pia stadi za kutoa taarifa kwa mitandao sahihi pindi wanapokumbwa na visa vya aina hiyo. Tangu mwaka 2013 jumla ya vikundi 43 vimeundwa kuhamasisha na vinajumuisha wanawake, vijana, viongozi wa mitaa na wale wa kidini.

Katika maeneo ambako wapiganaji wa zamani wa kikundi cha waasi wa FDLR wamejisalimisha, MONUSCO na kikosi cha serikali wanasaidia wapiganaji hao wa zamani na familia zao katika kuimarisha ulinzi wao na kuwakwamua kimaisha. Wapiganaji hao wamewekewa kambi zao kwenye maeneo ya Kayanbayonga,Walungu na Kisangani. Pichani familia za wapiganaji zikisindikizwa kuhakikisha usalama wao.

Mtoto wa kiume akishiriki kwenye igizo la sanaa la kuhamisisha na kuelimisha kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kingono unaoweza kufanywa na watendaji wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Hapo ni Sake jimboni Kivu Kaskazini na wanapatiwa stadi za kuhakikisha kuwa wana uwezo wa kuripoti tukio la aina hilo na wanafahamu ni wapi pa kuripoti ili hatua ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo.

Vijana wakazi wa eneo la Nyiragongo, huko Munigi jimboni Kivu Kaskazini wakiwa kwenye shughuli za kilimo, ikiwa ni moja ya miradi ya kupunguza ghasia kwenye jamii inayoendeshwa na MONUSCO na kusimamiwa na shirika la kiraia la ASDI mjini humo. Kupitia miradi hii ya kilimo vijana wanajipatia kipato na hivyo kuondokana na fursa au ushawishi wa kutumikishwa kwenye vikundi vilivyojihami ambavyo vinaleta ghasia.

Wakazi wa wa Munigi wakiwa katika tukio la uzinduzi wa kampeni ya kupunguza ghasia kwenye jamii katika jimbo lao hilo la Kivu Kaskazini ambako vikundi vilivyojihami vimekuwa chanzo cha ghasia huku wanawake na vijana wakishindwa kutekeleza shughuli zao za kujipatia kipato. Miradi hii ikiwemo kilimo, ushoni inaleta kuinua kipato na inatekelezwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO.