Watoto wakifuatilia kwa makini huku vicheko na tabasamu vikiwa wazi kwenye vinywa vyao wakati wa ufunguzi wa kituo chao huko Mathare. Gerry Lumumba(hayuko pichani) ndiye alikuwa mshereheshaji akiwaeleza watoto kuwa hii ni sehemu yenu, ni kona ya watoto.
Punde baada ya watoto kuelezwa kuwa ni kituo chao ni eneo lao, furaha iliwajaa na wakaanza kucheza muziki ambao ulikuwa unaporomoshwa kwenye kituo hicho kilichopo uwanja wa mpira wa Mlango Kubwa. Watoto walifurahi waliposikia ya kwamba, "kwa hiyo wakati wowote mnapotaka, au wakati wowote ambao utaona aibu, unaweza kuja hapa na kucheza hapa ni pahala penu," alisema Gerry Lumumba mshereheshaji wa tukio hilo.
Watoto walicheza na kufurahia na ndipo naye Mnadhimu Mkuu wa UN-Habitat, Kazumi Ogawa akapata fursa ya kuzungumza akisema kuwa "tunahitaji sehemu zaidi kama hizi kwenye jamii yetu. Pahala ambapo watoto na familia zao wanaweza kuwa salama kupumzika, kujilawaza na pengine hata kufanya sherehe."
Watoto wa kike na wa kiume walisikiliza kwa makini wakifahamu kuwa sasa angalau wakiwa Mathare jijini Nairobi nchini Kenya, wanaweza kupata pahala salama pa kucheza. UN-Habitatu inaamini kwa sehemu kama hizo maeneo ya mijini ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa watoto na vijana,
Mradi wa UN-Habitat unaotekelezwa duniani kuhusu sehemu salama za umma, unalenga kuboresha ubora wa maeneo ya umma ulimwenguni kote. Maeneo ya umma ni maeneo ambayo yanapaswa kufikika na watu wote, na maeneo hayo ni pamoja na bustani, mitaa, viambaza na maeneo ya michezo. Maeneo mazuri na salama ya umma yanasaidia kuimarisha utangamano pamoja na afya, furaha na ustawi wa wananchi wote.
Mbao ziliozumika kwenye ujenzi wa eneo hili salama na rafiki kwa watoto pamoja na muundo wake, zilikuwa zimetumika kujenga kibanda cha Sweden kilichokuwa kwenye maonyesho wakati wa Baraza la Mazingira duniani mjini Nairobi, Kenya. Mbunifu ramani za majengo, Ivan Segato kutoka ARVET amesema "hatukuweza kubeba mbao zetu kutoka Sweden ili kuonyesha ubunifu wetu, bali tulitembelea mafundi seremala hapa Nairobi tukapata mbao na kujenga kibanda chetu, na mwisho wa mkutano tukaona ni vyema kukabidhi jengo letu kwa kikundi cha kuhifadhi mazingira cha vijana kwenye eneo la Mathare.