
Mgogoro tu ulipoanza, tulinunua na kusambaza vikasha vya utu vyenye nembo ya UNFPA vikiwa na vifaa vya kawaida lakini muhimu kama vile chupi safi, sabuni na taulo za kike. Kwa wanawake ambao walikuwa wanahamisha familia zao hadi ugenini, jambo ambalo wasingalipenda liwakumbe ni kujisikia aibu kwa kuwa mwanamke. Hadi sasa wakimbizi 114,000 wanawake warohingya wamepatiwa vikasha hivi.

Kambi za Rohingya zilijengwa katika eneo ambalo lilikuwa ni msitu na hakukuwepo na jengo lolote. Tulijenga maeneo haya salama na rafiki kwa wanawake ambayo warohigya wanaita ‘shanti khana” au “ nyumba za amani” ili kutoa nafasi kwa wanawake kuzungumza na wafanyakazi wetu, kuzungumza pia na wananwake wenzao au kuwa na nafasi tulivu ya kutafakari wao wenyewe. Jengo lenye kituo rafiki cha 20 katika wilaya ya Cox’s Bazar karibu linakamilika na mamia ya wanawake wanatumia maeneo hayo kila siku.

Tulileta wataalamu wa afya ya akili , saikolojia na jinsia katika kipindi muhimu sana- punde tu baada ya kutokea mgogoro na baada ya watu kuanza kukumbwa na msongo wa mawazo na kiwewe.
Wataalam hawa sasa wamewapatia mafunzo wafanyakazi kutoka Bangladesh na ndani ya jamii ya warohingya wenyewe jinsi ya kutoa usaidizi wa tatizo la kisaikolojia na afya ya akili. Wafanyakazi wetu waliopatiwa mafunzo wamepata sifa za juu kabisa bila hata kupata shahada ya elimu ya juu. Wataalam wetu wako tayari wakati wowote kusaidia hata kisa kigumu zaidi. Mfumo huu uliowekwa mapema unamaanisha kuwa maelfu ya wanawake wameanza kupata nafuu ya kiwewe walichokuwa nacho na sasa wanaweza wakafikiria mustakhbali wao na kukabiliana na vizuri na changamoto yoyote ile.

Kati ya watu 700,000 waliowasili Bangladesh tangu mwezi Agosti mwaka jana, takriban 30,000 walikuwa wanawake wajawazito. Karibu kizazi kizima kipya kimezaliwa katika kambi kubwa zaidi duniani ya wakimbizi. Tumeajiri na kutuma wakunga wenye ujuzi wapatao 100 ili kuhakikisha kuwa mama na mtoto sio tu wanabaki hai lakini pia wanakuwa na afya njema . Hadi sasa takriban watoto 4,000 wamezaliwa katika vituo safi na salama vinavyopata msaada kutoka UNFPA. Wakunga wetu ndio wafanyakazi wetu walio mstari wa mbele, lakini pia wanasaidiwa wana madaktari wakiwemo wale wa watoto na madaktari wa wanawake ambao wanafanya upasuaji wa dharura wa uzazi iwapo utahitajika. Pia tumeleta wafamasia ili wasaidie huduma kubwa ya utoaji dawa inayohitajika.

Wanawake wote ambao ni wajawazito tunawapatia “kifurushi salama cha uzazi”cha kuwasaidia wakati wa kujifungua, ili mjamzito huyo asipokwenda kliniki na kuamua kujifungulia nyumbani kwake basi awe na vifaa muhimu kama vile shuka safi, taulo, vitambaa safi na pia kiwembe kisafi kwa ajili ya kukata kitovu cha mtoto. Mtoto akizaliwa , mama hupewa “kifurushi mama”ambacho kina nguo za mtoto, blanketi, nepi pamoja na vifaa vingine vya kujifasi kwa ajili ya mama. Tunataka kuzaliwa kwa mtoto kuwe ni sherehe na wala sio mzigo wa kifedha.

Tumeajiri wahudumu wa afya ya jamii 130, wengi wao ni wakunga wa jadi – ili waende katika jamii, kutambua wanawake wajawazito na kuwapatia ushauri wao na pamoja na familia zao kuhusu umuhimu wa kujifungulia mtoto chini ya msaada wa mkunga mwenye ujuzi. Wafanyakazi hawa wa kujitolea hivi sasa viongozi wanaoheshimiwa katika jamii na wanajibika na jukumu la kuokoa maisha ya wengi kwa kuwahimiza wanawake kwenda kliniki. Mpango wetu wa kujitolea, ambao kwao wanaojitolea wanapokea posho kwa kazi yao, utaongezeka maradufu miezi ijayo. Bado kuna maelfu ya wanawake ambao hujifungulia watoto wao majumbani na hivyo kuhatarisha maisha ya watoto wao -Tunataka kuwafikia wote hao.