Nchini Sudan Kusini, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS unasaidia kuimarisha doria kwenye maeneo ambayo bado yanakumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ikiwemo maeneo ya watu wa jamii ya asili. Lengo ni kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kawaida na hata akina mama kuweza kunyonyesha watoto wao.
Umoja wa Mataifa kwa kutambua umuhimu wa jamii za watu asili, umeunda jukwaa lao maalum ambalo hukutaka kila mwaka mara moja kujadili masuala yanayogusa siyo tu jamii hizi bali pia utangamano wao na jamii nyingine. Pichani ni mwaka 2016 wakati wa ufunguzi wa mkutano wao wa 15 maudhui yalikuwa Watu wa asili:Mizozo, amani na maazimio
Kila kabila lina utamaduni, na vivyo hivyo kwa jamii ya watu wa asili ambao pichani wanatoka jamii ya watu wa asili ya aborijini huko Australia. Hapa walikuwa wanacheza ngoma yao wakati wa tukio la kitamaduni kwenye uzinduzi wa mwaka wa watu wa asili katika moja ya kumbi za makao makuu ya Umoja wa Mataifa.
Jamii za watu wa asili zina mchango mkubwa katika amani na usalama duniani na ndio maana mwaka huu wa 2018, wakati wa mkutano kuhusu amani na usalama duniani na kushughulikia athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, Hindou Ibrahimu (pichani) mwakilishi wa watu wa asili kutoka Chad, alihutubia Baraza la Usalama kuelezea athari wanazokumbana nazo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Kabila la wamasai walioko eneo la Afrika Mashariki, linatambulika sana kwa kutunza na kuhifadhi utamaduni wao, iwe ni mavazi, chakula na hata ngoma. Pichani ni wamasai kutoka Kenya wakiwa katika moja ya vikao vyao vya kupashana kuhusu mila, desturi na kanuni zao. Vikao hivi hujumuisha wazee na vijana.
Watu wa jamii ya asili wana shughuli zao za kujipatia kipato. Pichani ni mwanamke mkazi wa Sin Chai nchini Vietnam akiwa kazini. Kabila lake ni la Hmong na wanaishi zaidi maeneo ya milimani. Kazi zinazofanywa na wanawake huchangia theluthi mbili ya kilimo cha chakula kwenye nchi zinazoendelea lakini bado hawana haki ya kumiliki ardhi.