Mtoto wa Esha, Ulensa akiwa amefikiwa na huduma ya kiliniki inayotolewa na kikosi tembezi cha huduma jumuishi za afya. Huduma hizi pamoja na ile ya kupatiwa mlo bora zimemfanya Ulensa mwenye umri wa mwaka mmoja kuwa na afya bora kuliko nduguze wawili kwani wao hawakunufaika na huduma hizo ikiwemo ushauri wa lishe kwa mtoto.
Ngamo Armando, amehakikisha mtoto wake Aive Afonso mwenye umri wa miezi 9 ananufaika na huduma za kijamii za afya jumuishi. Aliona mwanae anakohoa akaona bora amlete kwa vipimo na kisha akabainika ana utapiamlo. Sasa anapata nafuu baada ya kupatiwa uji wa karanga, wenyewe kijijini hapa wakiuita ‘chokoleti.’ Ngamo anashukuru uwepo wa huduma hii kwani hahitaji kwenda mwendo mrefu kupata huduma ya afya.
Wahudumu wa kiafya wa kijamii ndio wako mstari wa mbele kusaidia watoto na familia zilizofurushwa na machafuko yaliyoanza Cabo Delgado mwaka 2017. Hapa wanapatiwa mafunzo ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa mama na mtoto yanayotolewa na UNICEF kwa msaada wa ubalozi wa Ireland.
Baada ya mafunzo, akina mama wanapatiwa vifurushi hivi na ndoo vyenye vifaa sio tu vya kujisafi lakini pia vyakula vyenye lishe kwa ajili ya watoto hao waliokumbwa na utapiamlo kutokana na uhaba wa chakula kwenye eneo hili la Cabo Delgado lililokumbwa na machafuko tangu mwaka 2017.