Dieudonné Mugenyi yeye alifurushwa na mapigano akakimbilia eneo la Lambada jimboni Ituri. Baada ya kupatiwa mafunzo na SOFEPADI sasa anasimamia kitalu cha miche ya kabichi. Kila mwaka wanavuna tani 5000 za mazao ya mboga mboga na kumpatia kila mmoja dola 60 kwa mwezi.
Panga mkono wa kushoto, na mkono wa kulia ukipalilia bustani ya kabichi, ni Joseph Lonjiringa aliyekimbia mapigano eneo la Djugu, na kuishia hapa Bunia jimboni Ituri, nchini DRC ambapo mradi wa SOFEPADI umemletea tena matumaini ya kupata kipato na kusongesha maisha yake.
Uroci Pierre alisaka hifadhi Bunia baada ya waasi wa CODECO kushambulia kijiji chao. Anapalilia shamba la nyanyachungu akiwa na matumaini ya mavuno karibuni na kisha ajipatie fedha. Mradi huu unafadhiliwa na Muungano wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na SOFEPADI.