Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mataifa ya KiAfrika na FAO yaahidi kuimarisha elimu vijijini

Mataifa 11 ya KiAfrika, yalikutana karibuni mjini Rome, Utaliana kwenye Makao Makuu ya Shirika la UM la Chakula na Kilimo (FAO) na yaliafikiana kushiriki kwenye ule mradi wa kuimarisha elimu ya msingi vijijini, kwa dhamira ya kusaidia wakazi wa maeneo hayo kujipatia ujuzi wa kupiga vita, kwa mafanikio, ufukara, matatizo ya njaa, utapia mlo na kutojua kusoma na kuandika. Maafa haya ya kijamii huathiri zaidi mataifa ya Afrika yaliopo kusini ya Sahara.

"Jamii ya kimataifa yawajibika kuisaidia Afrika kutatua matatizo ya mipaka" - Ban Ki-moon

Katika risala aliyotuma kwenye Warsha wa Umoja wa Afrika Kuzingatia Suluhu ya Mizozo ya Mipaka, uliofanyika Disemba mosi nchini Djibouti, KM Ban Ki-moon alitoa mwito maalumu wenye kuihimiza jumuiya ya kimataifa kupania kuzisaidia nchi za Afrika kusuluhisha matatizo ya mipaka kwa taratibu za kuridhisha na kudumisha mistari halali ya mipaka yao na, hatimaye, kujiepusha na hatari ya kutumia masuala hayo siku za usoni kama kisingizio cha kufufua tena mapigano na vurugu kwenye maeneo yao.

MONUC yawataka wapiganaji waasi kusalimisha silaha

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) limetoa mwito uliowahimiza wapiganaji waasi kusitisha mapigano na kusalimisha silaha, na kuchukua fursa hiyo ya baadaye kujiunganisha na mpango wa kitaifa utakaowachanganyisha, kwa utartaibu ulio halali, na maisha ya kawaida ya jamii nchini.

KM ahimiza utulivu wa kisiasa katika JAK

Ripoti ya karibuni ya KM Ban Ki-moon kuhusu hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK) imeelezea kwamba matayarisho yanaendelezwa kuitisha mjadala wa kisiasa utakaojumuisha vikundi vyote kuzingatia mzozo uliosababishwa na vitendo vya uchokozi wa waasi katika maeneo ya kaskazini-magharibi na kaskazini- mashari ya nchi.

Naibu KM apongeza utaratibu mpya wa kuimarisha amani Burundi

Naibu KM Asha-Rose Migiro majuzi alishiriki kwenye mjadala wa Kamisheni ya UM juu ya Ujenzi wa Amani uliofanyika Makao Makuu ya UM ambapo kulizingatiwa mfumo mpya wa kurudisha utulivu na amani Burundi. Katika risala yake mkutanoni Naibu KM aliipongeza Burundi kwa kujishurutisha kutekeleza mpango wa amani nchini baada ya mapigano ya zaidi miaka kumi kusitishwa.

Mwendesha Mashitaka wa ICC ameishtumu Sudan kukataa ushirikiano na Mahakama

Luis Moreno Ocampo, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya UM juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kwenye kikao cha hadhara kwamba kwa muda wa miezi 10 sasa Serikali ya Sudan imeshindwa kutekeleza pendekezo la Baraza la Usalama la kuwakamata raia wawili wa Sudan, Ahmad Harun na Ali Kushayb, na kuwapeleka Mahakamani Hague, Uholanzi baada ya raia hawa kutuhumiwa makosa ya jinai ya vita katika Darfur.

Mapigano Chad yakwamisha misaada ya kiutu kupelekewa umma muhitaji

Ofisi ya UM inayohusika na Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kuingiwa na wasiwasi mkuu kuhusu usalama wa wahamiaji wa Sudan 230,000 pamoja na wahajiri wa ndani ya nchi 180,000 nchini Chad kwa sababu ya kuselelea hali ya mapigano katika eneo la Chad mashariki. Vurugu hili, ilisema ripoti ya OCHA, linakwamisha huduma za dharura za kupeleka misaada ya kiutu inayohitajika kunusuru kihali umma huo.

UNICEF kuchanja watoto na wanawake 100,000 Somalia dhidi ya maradhi

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeanzisha huduma ya kuchanja watoto wachanga 47,000 walio chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wanawake 56,000 wanaoishi kwenye kambi za wahajiri wa ndani ya nchi ziliopo kwenye eneo la Mogadishu-Afgooye, katika Usomali. Huduma hii itasaidia kuupatia umma husika tiba ya kingamaradhi dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa mastakimu ya kawaida.

Hapa na pale

Katika tafrija ya kutathminia Mafanikio ya Mfuko wa Maendeleo ya MDGs mjini NY, Naibu KM Asha-Rose Migiro alisema kwenye risala yake kwamba Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yametubarikia “ramani ya aina pekee” kutumiwa kujenga ulimwengu bora na alitahadharisha, vile vile, kutopwelewa katika kuzitekeleza, kwa wakati, zile ahadi za kupunguza hali duni, njaa, maradhi na kutojua kusoma na kuandika katika nchi masikini kabla ya 2015.