Burundi
“Warundi wanahitaji kuchukua hatua ili kutuliza hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020 ili kuhakikisha kwamba hali haizoroti na kwamba tunaweza kuhakikisha kiwango cha ujumuishwaji kinachohitajika kuutekeleza.”
Smaїl Chergui, Kamisheni wa amani na usalama kwenye Muungano wa Afrika. (AU)
CHIMBUKO LA MZOZO
Machafuko nchini Burundi yalianza April 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutaka kuwania tena kwa mara ya tatu uongozi wa nchi hiyo.
Ghasia zilizofuatia jaribio la mapinduzi ya kijeshi Mei 2015, zilisababisha mamia ya watu kuuawa, maelfu kupoteza makazi yao, na baadhi ya watu 420,000 kukimbilia nchi jirani.
Tangu wakati huo, Burundi imekuwa ikijaribu kutafuta suluhisho la amani la mgogoro wa kisiasa kupitia mazungumzo baina ya raia wa Burundi ambayo yanaongozwa na kanda ya Maziwa Makuu na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Kwa wakati huu taifa hilo linajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2020.
HABARI ZA UN KUHUSU BURUNDI
Bofya hapa kupata habari za Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi.
MJUMBE MAALUM KWA BURUNDI
Kwa kuzingatia maazimio ya Baraza la Usalama 2248 (2015), 2279 (2016) na 2303 (2016), tarehe 5 Mei 2017 Katibu Mkuu alimteua Rais wa zamani wa Burkina Faso, Michel Kafando kuwa mjumbe wake maalum ili kutoa msaada katika juhudi za jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mazungumzo ya amani na kuratibu juhudi za Umoja wa Mataifa za kuendeleza mchakato wa kupata amani na maendeleo endelevu nchini Burundi.
Kikosi cha mjumbe maalum nchini Burundi kimekuwa kinashirikiana na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Muungano wa Afrika kama sehemu ya kundi la pamoja la kiufundi (JTWG) kuunga mkono mchakato ambao hapo kabla ulikuwa unaongozwa na mshauri maalum wa katibu mkuu, Jamal Benomar.
WAKIMBIZI
Tangu Aprili, warundi 428,351 wamekimbilia nchi jirani kufuatia ghasia za uchaguzi mkuu. Idadi hiyo ni ile iliyoratibiwa na mpango wa kikanda kuhusu wakimbizi wa Burundi na inajumuisha wakimbizi wa Burundi tangu Aprili 2015, pamoja na baadhi ya warundi 37,000 walioomba hifadhi katika kanda hiyo ya Maziwa Makuu kabla ya Aprili 2015.
Mbali na idadi hiyo ya wakimbizi , kuna warundi wengine 12,500 nchini Kenya, 4,800 Msumbiji, 3,600 Malawi, na 2,500 nchini Zambia ambao wanasaidiwa chini ya mipango ya nchi walimosaka hifadhi.
Wakimbizi wengine kutoka Burundi 23,000, ambao wameishi kwa miongo kadhaa nchini Tanzania hao hawapati tena msaada.