Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Profesa Ali Mazrui wa Chuo Kikuu cha New York-Binghamton juu ya msiba wa biashara ya utumwa

Mnamo tarehe 25 Machi 1807 Bunge la Uingereza lilipitisha sheria ya kupiga marufuku jahazi zote za Kiingereza kusafirisha, kile walichokiita, bidhaa ya wanadamu, yaani ile biashara ya kuvusha watu waliotekwa nyara makwao katika Bara la Afrika, na ambao walisafirishwa mataifa ya ng\'ambo ya Bahari ya Atlantiki kufanya kazi ya utumwa, hususan katika Amerika na Visiwa vya Karibian.

UM imeanzisha tena huduma za kihali baada ya fujo kufifia DRC

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti ya kuwa hali ya vurugu na mapigano yaliofumka karibuni mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), baina ya vikosi vya Serekali na wafuasi wenye silaha wa aliyekuwa Naibu-Raisi Jean-Pierre Bemba, imeanza kufifia wiki hii na kuyawezesha mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu fursa ya kuendeleza shughuli za kutathminia hali, kwa ujumla, na vile vile kukidhia mahitaji ya umma ulioathirika na mapigano.

Wapatanishi wa Darfur waonana na makundi ya Waarabu na wawakilishi wa jumuiya za kiraia

Mjumbe wa KM kwa UM kwa Darfur, Balozi Jan Eliasson wa Usweden akifuatana na Dktr Salim Ahmed Salim, Mpatanishi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU)kuhusu Darfur, wiki hii walikutana kwa mazungumzo mjini Khartoum na wawakilishi wa makundi ya makabila ya KiArabu, pamoja na viongozi wanaowakilisha jumuiya za kiraia, na kusailiana juu ya uwezekano wa kufufua tena mpango wa amani wa Darfur, kwa lengo la kukomesha haraka umwagaji wa damu kati ya makundi yanayohasimiana kwenye eneo hilo.

Baraza la Usalama linazingatia masuala ya amani katika Afrika

Baraza la Usalama lilikutana kwenye kikao maalumu wiki hii kuzingatia ushirikiano kati ya mashirika ya kikanda na UM, hususan Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU) kwa makusudio ya kuimarisha usalama na amani. Kikao kilitilia mkazo umuhimu wa kukuza ushirikiano huo na kuboresha uhusiano mwema kati ya UM na AU, kwa matarajio ya kuzuia ugomvi na mapigano yanayozuka mara kwa mara barani Afrika, na kusimamia kipamoja taratibu zinazotakikana kuleta suluhu ya kudumu ya migogoro husika.

Hapa na pale

Wakati KM Ban Ki-moon alipokuwa kwenye ziara ya Mashariki ya Kati mapema wiki hii, alichukua fursa hiyo na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Riyadh, Saudi Arabia, ambapo kwenye risala yake alitoa mwito wa kuhimiza viongozi wanachama wajitahidi kufanya kila wawezalo kuutekeleza ule Mpango wa Amani juu ya tatizo la Falastina na Israili, pamoja na kuwataka waongeze bidii zao vile vile katika kuipatia suluhu mizozo husika mengineyo katika Darfur, Sudan, Usomali na vile vile ile mizozo iliojiri katika Lebanon na Iraq. ~