Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

KM azungumza na waandishi habari juu ya ziara yake ijayo katika Sudan, Chad na Libya

Ijumanne, Agosti 28 (2007) Katibu Mkuu (KM) wa Umoja wa Mataifa (UM) Ban Ki-moon alikuwa na mazungumzo na waandishi habari katika Makao Makuu juu ya ziara yake katika mataifa ya Chad, Libya na Sudan kusailia kipamoja na viongozi wa mataifa haya juu ya taratibu zitakazosaidia kurudisha utulivu na suluhu ya kuridhisha kuhusu tatizo la Darfur. KM alianza mazungumzo kwa kuelezea sababu hasa zilizomhamasisha yeye binafsi kuamua kufanya ziara hii:

MONUC yajaribu kupatanisha makundi yanayohasimiana DRC

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) inajishirikisha katika jukumu, lisio rasmi, la kujaribu kupatanisha vikosi vya serekali vya FARDC na wafuasi wa Jenerali aliyetoroka jeshi, Laurent Nkunda. Huduma hii inafanyika katika jimbo la kaskazini-mashariki ya nchi.

Baraza la Usalama kuidhinisha maandalizi ya vikosi vya amani kupelekwa Chad na JAK

Baraza la Usalama limeipa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya idhini ya kuandaa ratiba halisi itakayozingatia uwezekano wa kupeleka, shirika, askari polisi na wanajeshi katika mataifa ya Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kuwapatia hifadhi bora raia walioathirika na mzozo uliodondokea maeneo jirani na Darfur, Sudan. Baraza la Usalama limependekeza kupelekwa vikosi vya ulinzi wa amani kwa mwaka mmoja kuwapatia hifadhi ya kihali wahamiaji na watu waliohajiri makwao na raia husika waliopo Chad mashariki na kaskazini-mashariki ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK), na vile vile kuhakikisha wanapatiwa misaada ya kiutu kwa wakati.

Mazungumzo ya upatanishi ya Mogadishu kupongezwa na Mjumbe wa KM kwa Usomali

Francois Lonseny Fall, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali akiongoza ujumbe wa Kamati ya Ushauri ya Kimataifa Alkhamisi walihudhuria mjini Mogadishu taadhima za kufunga Mkutano wa Upatanishi wa Taifa. Fall aliwapongeza wawakilishi wote walioshiriki kwenye mkutano ambao alisema ulimalizika kwa mafanikio ya kutia moyo, kwa sababu ya mchango wa serekali umma wa Usomali ambao pamoja waliamua kuwasilisha suluhu ya kizalendo.

Raia wa Uchina kuongoza vikosi vya amani vya UM

Meja-Jenerali Zhao Jingmin wa Jamhuri ya Umma wa Uchina ameteuliwa na KM Ban Ki-moon kuwa Kamanda Mkuu mpya wa vikosi vya ulinzi wa amani vya UM katika Sahara ya Magharibi (MINURSO). Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa raia wa Uchina kuongoza operesheni za ulinzi wa amani za UM duniani.

UNICEF yasaidia waalimu Zimbabwe kudhibiti UKIMWI

Waalimu 1,500 wa skuli za msingi na sekandari nchini Zimbabwe walishiriki kwenye mafunzo maalumu ya wiki moja kwa lengo la kuilimisha wanafunzi 500,000 juu ya taratibu kinga dhidi ya hatari ya kupatwa na VVU na UKIMWI. Mafunzo haya yaliweza kufanyika kutokana na msaada wa dola 500,000 uliofadhiliwa na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF).

Hapa na pale

Wiki hii mjini Oslo, Norway kulifanyika mkutano maalumu, uliosaidiwa na UM, kujadilia ujuzi wa kisasa wa kutumiwa kuwasilisha Mapinduzi ya Kilimo Afrika, huduma ambayo itakuza mavuno na kuimarisha kilimo kwa umma.