Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Ripoti ya mfumo wa vikosi vya amani kwa Darfur imekamilishwa

KM Ban Ki-moon amemtumia Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Mei, Balozi Zalmay Khalilzad wa Marekani na vile vile Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika (AU), ripoti yenye kuelezea, kwa ukamilifu, mfumo wa vikosi vya mseto vya AU na UM vinavyotazamiwa kupelekwa kwenye jimbo la Sudan magharibi la Darfur.

ICTR imeidhinisha hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya M. Muhimana

Korti Ndogo ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) iliopo Arusha, Tanzania imeidhinisha na kuthibitisha tena ile hukumu ya 2005 ya kifungo cha maisha kwa Mikaeli Muhimana aliyetuhumiwa kuendeleza makosa ya jinai dhidi ya utu katika Rwanda mnamo 1994. Miongoni mwa makosa yaliyomtia hatiani Muhimana ni pamoja na kushtakiwa kushiriki kwenye jinai ya mauaji ya halaiki, vitendo vya kunajisi kihorera wanawake wawili na vile vile kumwua mwanamke mwengine mja mzito.

Vikosi vya MONUC katika DRC vinachunguzwa kuhusu rushwa

Ofisi ya UM ya Kuchunguza Ukiukaji Kanuni za Kazi (OIOS) imeripotiwa kuendeleza ukaguzi wa hali ya juu kuhusu yale madai kwamba vikosi vya ulinzi wa amani vya UM katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo vya Shirika la MONUC, vilihusika na biashara ya magendo ya madini katika kipindi kati ya miaka ya 2005-2006. Tuhuma zilidai vikosi vya MONUC vilinunua madini ya thamani kwa kuwapatia wachuuzi madini hayo silaha, biashara inayodaiwa kuendelezwa kwenye mji wa Mongwalu, Wilaya ya Ituri iliopo Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Chuo Kikuu cha Pretoria kupokea Tunzo ya UNESCO ya 2006

Taasisi ya Haki za Kibinadamu ya Chuo Kikuu cha Pretoria (Afrika Kusini) imetunukiwa Tunzo ya UNESCO ya 2006 kwa mchango wake wa kusaidia kuandaa Mswada wa Sheria ya Haki za Binadamu na pia kutayarisha Katiba mpya ya taifa baada ya ubaguzi haraka wa rangi kufyekwa nchini.

Hapa na pale

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Ulinzi wa Haki za Binadamu Duniani, Louise Arbour ameshtumu vikali muongezeko wa vurugu na mapigano yaliofumka karibuni kwenye Tarafa ya Ghaza, na ametoa mwito maalumu wenye kuhadharisha pande zote husika na mgogoro huu kutokiuka kanuni za kiutu za kimataifa, sheria ambazo zinawajibisha wenye madaraka kuhakikisha raia wote wanaojikuta wamenaswa kwenye mapigano kupatiwa hifadhi.~

Mazao ya nafaka 2007 kuvunja rikodi: FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) linaashiria uzalishaji wa mazao ya nafaka duniani kwa 2007 utavunja rikodi na kuongezeka kwa asilimia 5. Jumla ya mazo ya nafaka inabashiriwa kufikia tani milioni 2,095.