Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Baraza Kuu laahidi kujenga ulimwengu salama kwa watoto

Baraza Kuu la UM Alkhamisi limepitisha kwa sauti, na kauli moja, azimio la msingi ambalo Mataifa Wanachama yameahidi kukamilisha malengo ya kuendeleza maisha bora kwa watoto, hasa katika kuwapatia afya na elimu yenye natija kimaisha, na kuwapatia hifadhi inayofaa dhidi ya unyanyasaji, mateso na utumiaji nguvu, na pia kuwahakikishia udhibiti bora na tiba kinga dhidi ya UKIMWI/VVU.

KM ahimiza mataifa yakubaliane na ajenda ya Bali

Kwenye Mkutano Mkuu wa UM juu ya Udhibiti wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa duniani, unaofanyika Bali, Indonesia KM Ban Ki-moon alitahdaharisha wajumbe wa kimataifa kwamba suala la athari zinazoletwa na mabadiliko ya hewa ni "tatizo linalotatanisha sana maadili halisi ya vizazi vya leo" na kwamba tusahau "macho yote ya ulimwengu yanasubiri kuona hatua gani za kuridhisha zitachukuliwa na jamii yetu kulisuluhisha tatizo hili kuu la karne ya sasa."

Ripoti ya KM yasema "unyong'onyevu" wa maisha umetandaa Guinea-Bissau

Katika ripoti ya karibuni ya KM juu ya Guinea-Bissau ilibainishwa kwamba katika miezi michache iliopita imeonesha kuwepo muongezeko wa hisia za mzoroto wa maendeleo ya jamii nchini, mwelekeo ambao uliharibiwa zaidi na imani ya raia kwamba taasisi za kuendesha shughuli za taifa hazina dira ya mwongozo na zinaelea huku na huko dhidi ya maslahi ya umma.

Mjumbe Maalumu wa UM ameahidi kuongeza kasi kuwasilisha amani Darfur

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Darfur, Jan Eliasson aliwaambia waandishi habari mjini Khartoum, Sudan kwamba Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika watajitahidi sana, katika wiki chache zijazo, kuongeza kasi ya mashauriano yatakayosaidia kuharakisha mazungumzo ya kurudisha utulivu na amani kati ya Serikali ya Sudan na makundi kadhaa ya waasi kutoka jimbo la magharibi ya nchi la Darfur.

Mapigano katika Mashariki ya JKK yautia wasiwasi UM

KM wa UM Ban Ki-moon ameripoti kuingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama na amani ya raia wanaoishi kwenye eneo la Kivu Kaskazini, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), baada ya kufumka mapigano huko yalioselelea katika siku za karibuni. Alisema KM hali hii ya vurugu inakithirisha mateso na usumbufu wa kimaisha kwa raia, kijumla.

Siku ya Kupiga Vita UKIMWI Duniani humaanisha nini katika 2007?

Tarehe mosi Disemba huadhimishwa kila mwaka na Mataifa Wanachama, kuwa ni Siku ya Kupiga Vita UKIMWI Duniani ambapo walimwengu hukumbushana juu ya jukumu linalowasubiri kukabiliana na janga hili hatari la afya. Taadhima za mwaka huu zimetilia mkazo zaidi umuhimu wa kuwa na ‘uongozi bora’ katika kukamilisha ahadi za kuutokomeza UKIMWI ulimwenguni.

Mkutano wa Bali kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa waonesha dalili za kutia moyo - kumbukumbu

Kuanzia mwanzo wa wiki, wajumbe zaidi ya 10,000 wakiwakilisha nchi wanachama karibu 190, pamoja na waangalizi wa mashirika ya kiserekali na yasio ya kiserekali, na vile vile waandishi habari, walikusanyika Kisiwani Bali, Indonesia na kushiriki kwenye mijadala, itakayoendelea kwa majuma mawili, hadi Disemba 14, kuzingatia ajenda ya msingi wa mashauriano kuhusu Mkataba mpya wa kuimarisha udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani katika siku za usoni, hususan baada ya Maafikiano ya Kyoto kukamilisha muda wake katika 2013. Mashaurianio ya kimataifa kuhusu Mkataba mpya baada ya Maafikiano ya Kyoto yanapangwa kukamilishwa 2009.