Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Neno La Wiki

Neno la wiki: MEDE

Katika neno la wiki tunachambua neno "Mede", mchambuzi wetu leo ni Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Maswala ya Mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA.

Mede ina maana mbili, moja ni sehemu ya nyumba ambayo imetengwa kwa ajili ya kupumsikia,  yaani kupiga gumzi au kupumsikia na wageni maalumu kando na chumba cha kupumsikia na familia ya kwako. Pili, Mede ni mchezo wa watoto wa kujificha ili wenzake wamtafute, yaani wanaweza kujificha chini ya kitanda au sehemu nyingine ya siri.

Neno la wiki: FILA

Wiki hii tunaangazia neno "Fila" na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla Mhariri Mwandamizi, katika Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, nchini Tanzania.

Neno Fila ina maana mbili, ya kwanza neno hili hutumika katika msemo kwa maana ya "Ubaya" kwa mfano Lila na Fila haitangamani kumaanisha wema na ubaya havisikilizani, pili, Fila ni kifaa kinachotumiwa kujazia  wino kwenye mashine ya chapa.

Neno la Wiki- Mende

Katika neno la wiki Disemba 2 tunachambua neno Mende, mchambuzi wetu leo ni, Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa masuala ya mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA.

Bwana Bakari anasema mende ni jamii ya mdudu ambaye amegawanyika kwa sehemu tatu, mende huyo anachukua majina tofauti kulingana na mazingira aliyomo, kombamwiko akiwa jikoni, akiwa kwenye sehemu chafu ni mende na akiwa ni wa kike amebeba mayai ni nyenze.

Neno la wiki- Behewa

Wiki hii tunaangazia neno Behewe na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla Mhariri Mwandamizi, katika Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, nchini Tanzania. Buhewa lina zaidi ya maana moja, maana ya kwanza ni mahali pa wazi katika nyumba, maana nyingine ni sehemu au ghala ya kuwekea bidhaa kisawa chake ni bohari na nyingine ni sehemu ya gari moshi ya kuchukuliwa abiria au bidhaa.

Neno la wiki- Budi na Mujibu

Katika Neno la Wiki hii  Novemba 11 tunaangazia maneno budi na mujibu na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania.

Bwana Sigalla anasema katika lugha ya kisawhili kuna maneno hayasimami peke yake na ni lazima yaanze na maneno mengine kwa mfano budi lazima lianze na kikanushi kama sina budi nalo mujibu lazima liambatane na ‘kwa’ yaani kwa mujibu wa

Neno la wiki- Mbulu

Katika neno la wiki tunachambua neno mbulu, mchambuzi wetu leo ni, Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Maswala ya Mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA. Neno mbulu kama anayvofafanua Nuhu Bakari lina maana ya tabia za kiwenda wazimu.

Neno la wiki- matumizi potofu ya wingi wa maneno

Katika Neno la Wiki hii  Oktoba 28 tunaangazia matumizi potofu ya wingi kwenye maneno yasiyopaswa kuwekewa wingi. Maneno hayo ni: uamuzi, kuboresha na saa. Mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania. Anasema kwamba vyombo vya habari na wanasiasa wamekuwa wakiyabebesha wingi maneno hayo wakati hamna wingi akitolea mfano maamuzi wakati neno hilo halipo. Maneno haya hayabebi wingi.

Neno la wiki- Mnywanywa

Katika neno la wiki tunachambua neno mnywanywa, mchambuzi wetu leo ni, Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Maswala ya Mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA. Neno mnywanywa kama anayvofafanua Nuhu Bakari lina maana mbili. Maana ya kwanza ni aina ya mti na nyingine ni sifa ya mtu ambaye anapenda kulalamika sana, aidha mtu asiyeridhika.

Neno la wiki- Mtaadibu

Katika neno la wiki tunachambua neno mtaadibu, mchambuzi wetu leo ni, Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Maswala ya Mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA. Neno mtaadibu kama anavyoelezea Nuhu ni sifa ya mtu mwenye adabu nyingi aidha mtu anayependa kuwasaidia watu.